OMBAOMBA 14 DAR KUREJESHWA MAKWAO...

Uongozi wa Jiji la Dar es Salaam unakusudia kuwarudisha makwao ombaomba 14 waliokamatwa hivi karibuni katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Ubungo (UBT).
Hayo yamethibitishwa na Meneja wa kituo hicho, Juma Iddi, baada ya ombaomba hao kukamatwa wiki iliyopita na kufikishwa kortini walikopatikana na hatia, na sasa watarejeshwa makwao.
Ingawa hakusema wanatoka katika mikoa gani nchini, alidokeza kuwa, kwa sasa ombaomba hao wamehifadhiwa eneo maalumu wakati utaratibu wa kuwasafirisha ukiandaliwa.
Alisema uamuzi wa kuwasafirisha watu hao umetokana na hukumu iliyotolewa na mahakama ambayo  iliamuru warudishwe makwao.
Iddi alisema watu hao watarudishwa nyumbani kwao kwa kulipiwa nauli na Mamlaka ya Jiji na kwamba  endapo watarudi tena Dar es Salaam watachukuliwa hatua kali zaidi.
Aidha Idd alisema hatua ya kukamatwa kwa ombaomba hao imetokana na operesheni maalumu ya kuwaondoa watu wote wanaoendesha shughuli zao bila ya kufuata sheria kituoni hapo.
Alisema operesheni hiyo inayokwenda kwa awamu imeanza na ombaomba na baadae itafuatia wapiga debe, wachafuzi wa mazingira, vibaka pamoja na kundi la watoto ambalo linaonekana kuongezeka katika kituo hicho siku hadi siku.
Kampeni hiyo inakumbushia msuguano mkali uliokuwepo baina ya ombaomba maarufu nchini, Mzee Paulo Mawezi maarufu kwa jina la Matonya ambaye kwa sasa ni marehemu aliyeisumbua mno Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kutokana na kurudishwa kwao, lakini mara nyingi akionekana tena na kudai alikwenda ‘likizo’.
Matonya aliyefariki mwaka huu, alipata umaarufu Dar es Salaam na Morogoro kutokana na staili yake ya kuomba fedha kutoka kwa wapita njia akiwa amelala chali huku mkono akiwa ameunyoosha juu kwa muda mrefu bila ya kutikisika hata kama jua ni kali kupita kiasi.
Enzi za uhai wake, aliwahi kusema aliifanya kazi hiyo kwa miaka mingi, tangu miaka ya 1960, yaani siku chache kabla ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, mwaka 1961 akitokea kwao mkoani Dodoma, hivyo kujiita ‘Mtoto wa Mjini’.

No comments: