Kamanda David Misime. |
Mkoani Mara, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mabuimelafulu wilayani Musoma Vijijini, Benedicto Masenga (42), amehukumiwa na Mahakama ya Mkoa wa Mara kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili na kumpatia ujauzito.
Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Faisari Kahamba, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Jonathan Kaijage, aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi ya muda mrefu na mwanafunzi huyo na hatimaye alimpa ujauzito.
Kaijage alidai mshitakiwa huyo alimpa ujauzito mwanafunzi huyo, ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mugango mkoani Mara, baada ya kumbaka kwa nguvu ofisini kwake Mei 2009 na kisha akaendelea kufanya naye mapenzi hadi mimba ilipogundulika ikiwa ya miezi mitano.
Kutokana na ushahidi huo, Hakimu Kahamba alimhukumu mtendaji huyo kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, ili liwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia na tabia kama hiyo, hasa kwa kuzingatia kuwa huyo ni mtumishi wa umma alitakiwa kuwa mfano kwa jamii.
Mwandishi kutoka Dodoma anaripoti kwamba wakati Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mabuimelafulu akihukumiwa jela miaka 30, Mwenyekiti wa Kijiji cha Malolo katika Wilaya ya Mpwapwa, Daudi Nyaulingo (38), anashikiliwa Polisi kwa kutuhumiwa kuiba dawa katika zahanati ya kijiji hicho na kwenda kuuza.
Mwingine anayeshikiliwa pamoja na Nyaulingo ni Crispian Nyakasonga (28), ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), David Misime, alisema baada ya kutuhumiwa kwa muda mrefu, rafiki yake Nyakasonga alikutwa na vidhibiti nyumbani kwake kijijini Desemba 6, mwaka huu saa sita usiku.
Kwa mujibu wa Kamanda Misime, awali Polisi kupitia mkakati wake wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi walipata taarifa za kuuzwa holela kwa dawa mbalimbali za binadamu katika kijiji hicho.
Alisema uchunguzi wa awali ulianza mara moja kuhusu taarifa hizo na matokeo ya uchunguzi huo, yalimhusisha mwenyekiti huyo na biashara hiyo.
“Wanakijiji katika eneo hilo walikiri kwamba Mwenyekiti huyo amekuwa akiuza dawa hizo mara kwa mara,” alisema Kamanda Misime.
Alidai kuwa, Mwenyekiti huyo amekuwa akifungua chumba cha kuhifadhia dawa katika zahanati hiyo na kuiba na kwenda kuziuza akiwa na mtuhumiwa mwenzake, Nyakasonga na alikuwa akifanya hivyo kwa kuwa ndiye mwenye dhamana ya kutunza funguo za chumba hicho.
Misime alisema Nyakasonga alipofanyiwa upekuzi nyumbani kwake, alikutwa na makopo ya dawa aina za Paracetamol, Piriton na nyingine za aina mbalimbali ambazo ni miongoni mwa zilizoibwa katika zahanati hiyo. Thamani ya dawa hizo hazijafahamika hadi sasa.
Kamanda Misime alisema upelelezi ukikamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara moja.
Alitoa mwito kwa jamii kwa kupitia mkakati wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi, kuendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa mbalimbali za wahalifu na uhalifu na kupambana na kero na vitisho vya aina mbalimbali.
No comments:
Post a Comment