TAMKO ZITO LA KARDINALI PENGO KWA WATANZANIA HILI HAPA...

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka Watanzania kuimarisha undugu na ujamaa bila kujali tofauti za dini wala itikadi za siasa ili wajenge familia ya Mungu.
Amesema watu wote ni sawa, kutokana na kuumbwa kwa mfano wa Mungu; na masuala mengine yametokea tu, hivyo undugu na ujamaa ukitawala na kuwa na familia ya Mungu, migongano haitakuwepo hata kama ni dini tofauti au itikadi tofauti za siasa.
Kardinali Pengo alisema hayo jana, alipokuwa akitoa salamu zake za sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, ambapo aliwasihi viongozi wa siasa na Serikali, kukumbuka kuwa wana jukumu la kuwaunganisha watu wote wenye mapenzi mema.
Aliwataka kuleta maendeleo ya watu wote, bila kupendelea dini moja na kuendesha siasa bila ubaguzi ili kuepuka ugomvi na mapigano nchini.
Pia, Kardinali Pengo aliitaka Serikali isiwavumilie watu wasiotaka kutekeleza wajibu wao wa uraia mwema na kutaka kustarehe kwa gharama za wengine, kwani sio watu wote wenye nia njema.
Alisema wale wasioikubali Serikali na kutaka kuvunja amani wanatakiwa kuchukuliwa hatua mapema ili kuhakikisha wananchi wengine wanaishi kwa undugu.
Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, salamu hizo kwa Watanzania na waumini wake, ni sehemu ya  salamu za Maaskofu kwa Afrika zilizotolewa katika Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika Rome Oktoba 7 hadi 28 mwaka huu.
Akizungumzia mchakato wa maoni ya Katiba unaoendelea, alitaka wananchi waachwe watoe maoni yao na kushauri wakati wa kuchambua na kuandika Katiba, itumike busara kwa kuangalia uzalendo na siyo wingi wa watoa maoni.
Alisema anaamini wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, watalinda nchi na kuwa na taifa moja lisilogawanyika kwa kuchambua maoni yenye manufaa kwa Watanzania, ili waendelee kuwa taifa linaloheshimika na kuheshimu mataifa mengine.
Alisisitiza kwamba kwa kuangalia mawazo ya walio wengi, Katiba nzuri kwa Watanzania haitapatikana na cha msingi ni kuchukua yale ya manufaa pekee.
Akizungumzia uwepo wa shule wanazosoma watoto wa wenye kipato kizuri na zingine wanazosoma watoto wa masikini, alisema mtoto wa masikini akikosa elimu, anakuwa masikini milele yote.
Alionya kuwa ubaguzi katika elimu ukiendelea ni sawa na  kujiandalia matatizo katika siku zijazo za mbele.
Alisema utafika muda, wale masikini na wenye hali ya chini watasema inatosha; “matajiri wanajirundikia mali wakati wao wanakufa kwa njaa; wamejenga hospitali zao zenye vifaa vyote vya matibabu pamoja na shule zao zinazotoa elimu bora.”
Alihadharisha kuwa siku hiyo ikifika, damu itamwagika kwa kuwa hawatakubali kuishi katika nchi yenye matabaka ya namna hiyo.
Kutokana na hali hiyo, amesema Kanisa Katoliki walianzisha shule za St Joseph Millennium kwa nia ya kutoa elimu bora kwa gharama nafuu bila kujali tofauti za dini au kipato cha watu.
Alisema ada wanayotoza ni kwa ajili ya gharama za msingi za kuendesha shule, ambazo kanisa haliwezi kuzibeba huku akisisitiza wale wenye uwezo kutoa gharama zaidi, ili  kusaidia wanafunzi ambao wazazi wao wana kipato cha chini.
Alisema shule zikiwa kitega uchumi, ndiyo chanzo cha matokeo ya kutoridhisha, kwani watoto wa matajiri watajazana huku wakifikiria mali za wazazi wao.
Alisema shule za madhehebu hazipaswi kuwa za vitega uchumi, ndiyo maana hakuna inayotoza ada zaidi ya zile ambazo ni za kitega uchumi na kusisitiza kuwa kama kuna shule ya Kanisa Katoliki inatoza ada hizo, ni vema aambiwe. Alisema akibaini kuwa ni kweli hatasita kuifunga shule hiyo. 
Aliitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya mihadhara ya kidini, inayotumiwa na dini moja kutukana nyingine, kwa kuwa hakuna  mwenye haki ya kumtukana mwenzake kwa sababu ya imani.
Alisema mihadhara hiyo, ikiendelea na mabishano yakizidi, kitakachofuata ni kupigana na kusisitiza kuwa tofauti za imani, hazina sababu ya kutukanana zaidi ya kuzungumza kitaaluma na kuelimishana kwa kuwa kila mmoja ana hoja kulingana na imani yake.
“Kama Serikali inashindwa kudhibiti mihadhara hiyo, imeshindwa kutekeleza wajibu wake kwani suala hilo la kutukana sasa limeingia hata katika siasa, ambapo wanasiasa hawajibu hoja jambo ambalo halisaidii Watanzania,” alisema.
Alionya Watanzania wasipojirekebisha, siasa pia inaweza kuwa chimbuko la mapambano na kusababisha vita na kusisitiza kuwa kinachotakiwa ni kujibu hoja katika siasa kwa manufaa ya wananchi.
Makanisa yaliyochomwa
Alizungumzia masuala mbalimbali ya uchomwaji wa makanisa yaliyotokea siku za karibuni na kutaka suala hilo liangaliwe kwa umakini, kwani linaweza kuwa sababu ya kugawa wananchi kwa Serikali yao.
Alisema hatua zilizochukuliwa zinaweza kuonesha kuwa Serikali iko kwa ajili ya dini au madhehebu fulani na kuongeza kuwa ni  hatari kuwabagua Watanzania kwa imani.

No comments: