MTENDAJI AFUNGWA kWA KUMKATA MASIKIO 'MGONI' WAKE...

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Malembeka, Kipa Kigombe (52) amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na  hatia ya kumkata masikio mwanamume mmoja aliyemkuta na mkewe, akamtuhumu kuwa ana ushirikiano naye wa kimapenzi.
Hata hivyo, Mtendaji huyo aliambiwa anaweza kuepuka kuanza maisha ya jela endapo atalipa faini ya Sh laki tano. Mpaka mwandishi anaondoka Mahakamani, Kigombe alikuwa hajalipa faini hiyo.
Ofisa Mtendaji huyo pia ameamriwa na Mahakama hiyo iliyokuwa inaketi mbele ya Hakimu Safina Simfukwe, kumlipa mlalamikaji Sh 300,000 kama fidia na kwamba ahakikishe analipa pesa hizo pale atakapomaliza kifungo chake (kama atakwenda jela kwa kukosa kulipa faini).
Awali mwendesha mashitaka katika Mahakama hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Masoud Mohamed, alisema kuwa Ofisa Mtendaji Kigombe alitenda kosa hilo  Januari 21, mwaka 2010, saa 6:30 mchana, baada ya kumkuta mwanamume mmoja Shaga Isaka, mkazi wa kijiji hicho nyumbani kwake akizungumza na mke wake.
Mohammed alisema baada ya Mtendaji huyo kumkuta mwanamume huyo katika mazingira hayo, alichomoa kisu na kumkata masikio yote mawili, akidai kuwa amemkamata ugoni. Kutokana na hatua hiyo mlalamikaji alifungua kesi Polisi na mtuhumiwa akakamatwa na kufikishwa katika Mahakama hiyo.
Kufuatia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka, Hakimu Simfukwe, alisema ameridhika pasipo kuacha shaka yoyote na hivyo mshitakiwa huyo anastahili adhabu hiyo ili liwe fundisho kwake, hasa ukizingatia kuwa yeye alikuwa mtumishi wa Serikali ambaye kimsingi anajua taratibu zote lakini akajichukulia sheria mkononi.
Wakati huo huo, Mahakama hiyo imemhukumu kifungo cha miaka saba jela Masumbuko Musimu (26), mkazi wa Musoma, kutokana na kosa la kuvunja nyumba moja ya kulala wageni ya Sapiwi iliyoko mjini Bunda na kuiba vitu mbalimbali.

No comments: