MWANAMKE AFA AKITOLEWA MIMBA TABORA...

Mwanamke mwenye umri wa miaka 36, Asha Damanya, mkazi wa Kijiji cha Mwamala wilayani Nzega, Tabora, amefariki dunia akifanyiwa zoezi la kutolewa mimba katika Zahanati ya Matina iliyopo Kata ya Nyasubi, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi  saa moja na robo usiku, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Onesmo Lyanga, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa  Damanya alifariki dunia wakati akitolewa mimba na Mganga wa Zahanati hiyo, Damas Matina (63).
Lyanga alisema taarifa za awali zinaonesha kwamba wakati wa harakati hizo kutolewa mimba, mwanamke huyo alianza kutokwa na damu nyingi na kujikuta akizidiwa na hali yake kuzorota  hadi kufikia hatua ya kupoteza maisha akiwa kwenye zahanati hiyo.
“Sisi kama Jeshi la Polisi mara tuliposikia taarifa hiyo tulikwenda kwa haraka na kumkamata mganga aliyehusika kufanya kitendo hicho na mpaka sasa yuko chini ya ulinzi na tunaendelea kuchunguza kifo hicho zaidi kama kuna jambo lingine lililoweza kumfanya hadi akapoteza maisha,” alisema.
Katika tukio jingine, mkazi mmoja wa Kijiji cha Iponyahoro Kata ya Sabasabini,  Andrew Michael (32), amekutwa amekufa huku mwili wake ukiwa karibu na shamba la jirani yake, Herman Magolane (28) na baiskeli ya marehemu ikiwa kando ya mwili wake.
Kaimu Kamanda Lyanga alisema mwili huo uligunduliwa na wapita njia  ambao walitoa taarifa katika Jeshi la Polisi.

No comments: