MSICHANA ALIYEBAKWA NA WAHUNI SABA AKATWA UTUMBO...

Mmoja wa waandamanaji akilaani vikali kitendo hicho mjini New Delhi.
Mwanafunzi mwenye miaka 23 ambaye alibakwa na genge la wahuni wasiopungua saba ameieleza familia yake anataka kuishi huku maandamano makubwa yakitawala katika mji mkuu wa India kulaani shambulio hilo.
Maelfu ya waandamanaji wamepambana na polisi baada ya kujaribu kuandamana kuelekea Ikulu mjini New Delhi, wakirusha mawe wakati mabomu ya machozi yakitupwa kujaribu kuwatawanya.
Ndani ya kitengo cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Safdarjung, muathirika huyo kijana amekuwa akiwasiliana na wazazi wake kwa mwandiko mbovu kwenye kipande cha karatasi wakati akipigania kubaki hai.
"Je, wabakaji hao wamekamatwa?" aliuliza Alhamisi iliyopita.
"Wanastahili kuadhibiwa" aliandika kwenye kipande kingine. Na kisha mwishowe akaandika, "Nataka kuishi".
Watuhumiwa sita wamekamatwa kufuatia shambulio hilo lililotokea Desemba 16 pale msichana huyo alipobakwa kwa kurudia rudia na kuingiziwa nondo wakati akiwa kwenye basi.
Analazimika kuondolewa utumbo wake na madaktari mwanzoni walikuwa na mashaka kama ataweza kusalimika.
Baada ya mapambano ya piga nikupige na polisi siku nzima, waaandamanaji hao waliwasha mishumaa na kusali.
Baadhi ya waandamanaji hao walibeba mabango yaliyosomeka "Okoa wanawake. Okoa India" na "Nyonga wabakaji hao".
V.K. Singh, mkuu wa jeshi la India mstaafu, aliungana na waandamanaji hao na kushutumu "siasa na ukatili dhidi ya wanawake."
Ametaka mabadiliko ya haraka kuwapa mafunzo polisi na vikosi vya ulinzi.
Tukio hilo la kutisha limeibua mjadala India nzima ambapo wengi wanataka adhabu ya kifo kwa wote watakaopatikana na hatia na sheria mpya kuwalinda vema wanawake.
Delhi inaongoza kwa uhalifu dhidi ya wanawake lakini kumekuwa na ongezeko la asilimia 20 katika kesi za ubakaji mwaka huu.
Mwaka 2011 kulikuwa na mashitaka 482 katika Delhi - iliyobatizwa 'mji mkuu wa ubakaji' - kulinganisha na matukio 582 mwishoni mwa Novemba na kuna kesi 350 zinazosubiria kusikilizwa.
Mkuu wa Polisi alikemea vikali vitendo viovu juzi baada ya kushauri wanawake wabebe unga wa pilipili kujikinga wenyewe na kuepuka kutoka wakati wa usiku.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Sushilkumar Shinde amesema polisi watano wa New Delhi wamesimamishwa kazi kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti kufuatia shambulio hilo la ubakaji.
Pia amekutana na ujumbe wa wanafunzi waandamanaji na kuwaasa kumaliza maandamano yao.
Singh amewaomba waandamanaji hao, ambao wengi wao ni wanafunzi, kuandamana kwa amani ili kuepuka uharibifu wa mali za serikali.
"Serikali inawasikiliza na kuchukua hatua zinazofaa kuhakikisha usalama wa wanawake," Singh aliwaeleza waandishi wa habari.
Shambulio hilo lilitokea baada ya msichana huyo na rafiki wa kiume, wote kutoka Uttar Pradesh, kupanda basi majira ya Saa 3:30 usiku baada ya kuwa wametoka kutazama sinema.
Mjomba wa mwanaume huyo alisema kwamba baada ya kuingia kwenye basi waliona watu wachache wakiwa wameketi ndani.
"Walikuwa takribani watu saba kwenye basi, ambao kwanza walianza kumchokoza," alisema. "Kisha walianza kumbughudhi kiasi cha yeye kujibu mashambulizi na kujizuia."
Wakiwa wamechukizwa na kujizuia kwake, wakampiga kwa nondo na vitu vingine vilivyokuwamo kwenye basi kabla ya kumchukua na kumpeleka msichana huyo sehemu ya mbele ya basi kisha kumbaka.
"Watu watano hadi saba walisashambulia wawili hao," mjomba huyo aliongeza. "Pale mpwa wangu alipojaribu kumwokoa msichana huyo, alipigwa na nondo, msichana huyo kisha akabakwa na genge hilo."
Vyanzo vimeeleza kwamba nguo zake zilikatwa kwa wembe ambao pia ulichana tumbo lake na kupigwa sehemu mbalimbali kichwani.
Mjomba wa mwanaume huyo aliendelea, "Nimeona ripoti ya matibabu. Inasema alibakwa mara mbili na kila mmoja na kisha waliwatupa kwenye sehemu ya faragha mjini Mahipalpur baada ya kuwapora vitu vyao vyote vya thamani zikiwamo simu za mkononi."
Kisha washambuliaji wakawavua nguo zote na kuwaacha uchi wawili hao na kuwatupa kando ya barabara.
Msichana huyo alifanyiwa upasuaji uliochukua masaa mawili Jumatano iliyopita kuondoa sehemu zilizoathirika kwenye utumbo wake na anasemekana kuwa 'anaendelea vizuri'.

No comments: