WAUA MWANAMKE BUTIAMA, WATOKOMEA NA KICHWA CHAKE...

Kamanda Absalom Mwakyoma.
Matukio ya kutisha ya kuchinjwa watu na kuondoka na vichwa au kunyonya damu, yanaendelea kushamiri wilayani hapa, baada ya mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina Tabu Makanya (68), mkazi wa kijiji cha Kwikuba, kuuawa na wauaji kuondoka na kichwa chake.
Tukio hilo ni la nne katika siku za hivi karibuni na kati ya waliouawa, watatu ni wanawake.
Kifo cha Makanya kilitokea Desemba 21, mwaka huu saa 5:30 usiku ambapo wauaji hao walifika nyumbani kwa marehemu na kumshambulia kwa kumpiga na fimbo na bapa za panga sehemu mbalimbali ili kumlegeza mwili wake na baadaye, wakamchinja na kuchukua kichwa chake kikiwa kwenye mfuko wa sandarusi.
Kutokana na kushamiri kwa matukio hayo wananchi na waendesha pikipiki waliandamana na kufika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, ambaye aliwatuliza akiahidi jeshi lake kuimarisha ulinzi shirikishi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda Mwakyoma alisema kuwa wauaji hao wameshajulikana, lakini majina yao yamehifadhiwa hadi watakapokamatwa.
"Baada ya kuondoka kwa wauaji hao nyumbani kwa marehemu ndipo vijana waliopo kwenye nyumba hiyo uwani pamoja na majirani walipiga yowe na kuanza kuwafukuza na baada ya kuona wanazidiwa walikitupa kichwa hicho na kutokomea gizani kwenye vichaka," alisema Mwakyoma.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa juhudi za kufuatilia wahusika zimeanza kwa nguvu zote, lakini hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa.
Matukio hayo ya watu kuchinjwa Wilayani Butiama yamefikia manne katika kipindi kifupi. Desemba 2, mwaka huu, mwanamke aliyejulikana kwa jina la Blandina Peru alichinjwa na kuchukuliwa damu yake tu, ambapo watuhumiwa watatu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
"Katika tukio hili tuliwakamata watuhumiwa watatu na wameshakiri kuhusika na tukio hilo. Hawa kwa majina ni Sura Siriro, Jani Magesa na Mgasa Nyarukama.
Tukio lingine alisema ni la mauaji ya Sabina Mkireri wa kijiji cha Kabegi, Kata ya Nyakatende wilayani humo na watu sita wamekamatwa na wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo," alisema.
Tukio jingine ni la mwendesha pikipiki, Thomas Majengo ambaye ni Mkazi wa Kiara Manispaa ya Musoma. Yeye alichinjwa kisha kunyang'anywa pikipiki yake.

No comments: