IGP APELEKA TIMU MAALUMU KUCHUNGUZA MAUAJI YA TRAFIKI WAWILI, RAIA...

Advera Senso.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Saidi Mwema amepeleka mkoani Kagera timu maalumu ya uchunguzi,  kuchunguza zaidi tukio la mauaji ya askari polisi wawili na raia mmoja yaliyotokea katika kijiji cha Mgoma, Tarafa ya Kanazi wilayani Ngara mwishoni mwa wiki.
Mauaji hayo yalitokea juzi kijijini Mgoma na waliokufa ni mwananchi Sande John na askari wawili, Koplo Pascal na Konstebo Alexanda.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, timu hiyo maalumu ya IGP Mwema kutoka Makao Makuu ya Polisi, inahusisha Idara ya Upelelezi na Kamisheni ya Operesheni na itaungana na timu ya Upelelezi ya Mkoa wa Kagera katika uchunguzi huo.
“Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Saidi Mwema amepeleka mkoani Kagera timu maalumu ya uchunguzi kutoka Makao Makuu ya Polisi, inayohusisha Idara ya Upelelezi na Kamisheni ya Operesheni, ili kuungana na timu ya upelelezi ya Mkoa kuchunguza zaidi tukio hilo na kuwabaini wote waliohusika katika kusababisha vifo kwa askari na raia pamoja na madhara mengine dhidi ya mali,” ilisema taarifa ya Senso.
“Wakati uchunguzi huo ukiendelea, Jeshi la Polisi linawaomba wananchi kuwa watulivu, hususani wananchi wa Mkoa wa Kagera na waendelee kutoa ushirikiano wa dhati kwa Jeshi la Polisi ili wahalifu hao wachache wanaotumia kisingizio cha hasira kali waweze kukamatwa na sheria kuchukua mkondo wake,” iliongeza.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kagera, askari hao waliuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kukatwa katwa mapanga, baada ya askari polisi kumuua raia mmoja kwa kumpiga risasi kifuani na mguuni. Mamia ya wananchi walivamia Kituo cha Polisi cha Mgoma na kukichoma moto.
Habari kutoka katika eneo la tukio na zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Philip Kalangi zilisema askari hao wamekufa baada ya kushambuliwa na mamia ya wananchi waliovamia kituo hicho cha polisi kwa lengo la kuwaua askari hao, ambao ni wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Ngara.
Shuhuda mmoja aliliambia gazeti hili, kuwa askari hao walifika katika eneo hilo kwa lengo la kukamata pikipiki moja, iliyokuwa kwa fundi, Said Konikoni ambayo inadaiwa kuwa dereva wake alikuwa anakabiliwa na kosa la usalama barabarani.
“Walipofika kwa fundi huyo ambaye wakati huo alikuwa akitengeneza pikipiki hiyo, walilazimisha kuichukua, lakini fundi alikataa na ndipo mmoja wa askari hao alipompiga ngumi usoni, ambapo kijana huyo alianza kujitetea kwamba yeye siyo mwizi huku akivutana na askari aliyempiga ngumi, ndipo yule aliyekuwa na bunduki akampiga risasi ya kwenye goti…’’ alisema shuhuda huyo na kuongeza.
“Baada ya kijana huyo kuanguka chini na kuanza kulia huku akipiga kelele za kuomba msaada, askari huyo akampiga risasi nyingine kifuani na kufa papo hapo, kisha askari hao wakakimbilia kituoni…”
Alisema kwa kuwa juzi ilikuwa ni siku ya gulio katika eneo hilo, baada ya wananchi wa eneo hilo na wale waliokuwa wamefurika kwenye gulio kusikia mauaji hayo, waliandamana hadi kwenye kituo hicho huku wakiwa na galoni za mafuta ya petroli na kurusha ndani ya kituo hicho na kukilipua, ambapo askari wanne waliokuwepo wakiwemo wawili waliouawa. wakaamua kukimbia.
“Mmoja walimkamata hapohapo eneo la tukio na kumshambulia na kumuua papo hapo na kisha kumfuata mwingine ambaye alikuwa amekimbilia kwenye nyumba jirani na kujifungia, ambapo walimtoa ndani ya nyumba na kumshambulia kwa mapanga na mawe na kumuua papo hapo kisha wakaondoka katika eno la tukio huku wakiacha kituo kikiendelea kuteketea kwa moto,” alifafanua shuhuda wetu.

No comments: