JIKO LA MKAA LAUA WANAFUNZI WATATU WA FAMILIA MOJA TARIME...

Kamanda Justus Kamugisha.
Wanafunzi watatu wa familia moja katika Kijiji cha Nyangoto, Tarafa ya Ingwe wilayani Tarime Mkoa wa Mara, wamekufa kwa kukosa hewa ndani ya nyumba walimokuwa wamelala.
Wamekufa baada ya kuacha jiko la mkaa lililokuwa limeinjikwa maharage, likiwaka bila kuzima na wao kwenda kulala.
Waliokufa ni Naomi Nyasenso (14) wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyangoto, Magreth Nyasenso (10) wa darasa la nne na Debora Nyasenso (6) wa darasa la kwanza.
Aidha, mama yao baada ya kugundua kuwa watoto wake watatu wamefariki dunia, naye alikunywa sumu ili afe, lakini ameokolewa kwa kukimbizwa hospitali na kutapishwa sumu mwilini.
Akizungumza jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Kamishina Msaidizi Justus Kamugisha alisema vifo hivyo vilitokea juzi alfajiri nyumbani kwa baba yao.
“Tukio hili la watoto hao watatu, Naomi, Magreth na Debora wa familia moja ya Bwana Nyasenso ambao ni wanafunzi, ni la kusikitisha. Lilitokea Desemba 15, alfajiri nyumbani kwa Bwana Nyasenso ambapo ilidaiwa kuwa vifo hivyo vimetokana na kukosa hewa katika chumba walimokuwa wamelala ambacho kulikuwa na jiko la moto lililokuwa likipika maharage,  kusababisha kukosa hewa na kusababisha vifo kwa wanafunzi hao,” alisema Kamanda Kamugisha.
Kamanda Kamugisha aliiongeza, “Mama mzazi wa watoto hao kwa jina Bhoke Nyasenso, baada ya kugundua asubuhi kuwa wanawe wamefariki wote watatu, aliamua kunywa sumu ili naye afe, lakini  majirani na Jeshi letu la Polisi walifika na kumkimbiza Hospitali ya hapo Nyamongo.
“Alipatiwa huduma ya kwanza kwa kutapishwa sumu na kuwekewa maji ambapo kufikia Jumapili Desemba 16, amepata nafuu na kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo ndugu zake tumewataarifu kuwa karibu naye kwa uangalizi zaidi na kumfariji.”
Alitoa mwito kwa wazazi kuwa makini wakati wanapoacha moto ukiwa unawaka bila ya kuuzima na kuweza kuleta madhara kama hayo. Pia aliwashauri wananchi kujenga nyumba na kuweka madirisha makubwa, kwani nyumba hiyo ingekuwa na madirisha makubwa ya kuingiza hewa, ajali hiyo isingetokea.
Katika tukio jingine, wananchi wenye hasira katika Kijiji cha Kimusi Kata ya Nyamwaga, Tarafa hiyo ya Ingwe, wamemuua mkazi wa kijiji hicho, Mwita Reli kwa kumkata mapanga kwa tuhuma za wizi wa mifugo.
Pia, watuhumiwa wengine wa ujambazi wa kutumia silaha, Mwita Nyanokwe na Manyaka Ryoba na mwenzao huyo aliyeuawa, walichomewa nyumba zao.
Familia zao hazina makazi  kwa sasa na wamehifadhiwa na jamaa zao, ambapo watuhumiwa wengine wametoroka na Polisi inawasaka.

No comments: