TUSUBIRI KUSIKIA LOLOTE AFYA YA RAIS MUGABE...

PICHA KUBWA: Mugabe alipokuwa akisherehekea miaka 88 ya kuzaliwa kwake Februari mwaka huu. KULIA: Rais Robert Mugabe (juu) na 'Mrithi' wake, Emmerson Mnangagwa.
Gazeti la Mail la Zimbabwe limemnukuu mmoja wa maofisa wa chama cha ZANU-PF, akisema kuwa kiongozi wa chama hicho, Robert Mugabe, ambaye ameongoza nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1980, amekuwa akipatiwa matibabu ya kina saratani ya damu barani Asia.
Mugabe alienda nchini Singapore kwa ajili ya kumsajili binti yake, Bona kwenye chuo kikuu cha nchini humo.
Lakini usajili bado haujaanza mpaka Septemba na wapinzani wamesema ni makosa kwa yeye kusafiri nje ya nchi kushughulikia suala kama hilo yeye mwenyewe.
Vyanzo vya habari kutoka Iran, ambavyo vina mahusiano mazuri mno na Zimbabwe, vimesema Mugabe ameshaandaa mrithi wake. Pia familia yake imedaiwa kuwa imezingira kitanda wakisali kumwombea kiongozi huyo.
Gazeti la The tehran Times limesema Rais huyo amefikia uamuzi wa kiume kukasimu madaraka kwa Waziri wake wa Ulinzi, Emmerson Mnangagwa mwenye miaka 65, ambaye alisaidia vurugu za upinzani dhidi ya Waingereza miaka ya 1970.
Mkuu wa zamani wa usalama wa taifa Zimbabwe ameshutumiwa pia kuhusika kumsaidia Mugabe na kuvuruga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2008, ambapo mpinzani wake Morgan Tsvangirai, aliongoza kwenye kura mwanzoni.
Inadhaniwa pia alihusika kwa kiasi kikubwa kukisambaratisha chama cha upinzani cha ZAPU katika miaka ya 1980 na kusababisha maelfu ya raia wakipoteza maisha.
Hakukuwa na taarifa zozote kuhusu afya ya Mugabe hadi jana jioni kutoka kwa familia yake ama Serikali ya Zimbabwe.
Wasaidizi wa Mugabe walikanusha vikali kwamba kiongozi huyo anapatiwa matibabu ya dharura, wakidai kuwa kiongozi huyo anafurahia mapumziko ya Pasaka barani Asia akiwa na familia yake.
Lakini Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Joice Mujuru, ameripotiwa kukatisha ziara yake Asia na kurejea nyumbani kuandaa mazingira ya uwezekano wa kutokea kifo cha Mugabe.
Inafahamika kuwa Rais huyo ameenda mara nane nchini Singapore mwaka jana kwa ajili ya matibabu. Taarifa za kidiplomasia zilizosambazwa mwaka jana na mtandao wa Wikileaks zilisema Mugabe amegundulika na ugonjwa wa saratani mwaka 2008 na amekadiriwa kuishi kwa miaka mitano tu kutokana na saratani hiyo kusambaa mwilini.
Inasemekana alitupilia mbali ushauri kutoka kwa madaktari wake wa kuachia ngazi.
Mwezi Februari mwaka huu, Mugabe alisherehekea miaka 88 katika sherehe iliyofana kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Harare, ambayo inakadiriwa kugharimu Pauni za Uingereza 650,000.
Imeelezwa kuwa Rais huyo aliagiza alishwe keki yenye umbo la mamba.
Mugabe alichukuliwa kama shujaa miongoni mwa Waafrika wengi pale alipoingia madarakani miaka 32 iliyopita huku Zimbabwe ikitazamwa kama kioo cha mafanikio ya mabadiliko kutoka utawala wa watu weupe.
Lakini mafanikio hayo ya taifa hilo yamebadilika na kuonekana si kitu kutokana na jinsi taswira ya Mugabe ilivyobadilika.
Kwa sasa anatazamwa kama mvunjani mkubwa wa haki za binadamu duniani. Amedaiwa kuhusika na mauaji ya maelfu ya rais wake na kusambaratisha wapinzani wa utawala wake.
Sera zake mbovu pia zimeshutumiwa kuifilisi Zimbabwe. Mabadiliko aliyofanya ya umilikishwaji ardhi kwa wazawa kutoka kwa watu weupe, yameshutumiwa vikali na Serikali za Uingereza na Marekani.

No comments: