ALIYEMWAGIWA TINDIKALI MIAKA 12 ILIYOPITA AJIUA...

PICHA KUBWA: Younus baada ya shambulio. KATIKATI: Younus alivyokuwa kabla (juu) na Bilal Khar (chini). KULIA: Mazishi ya Younus wiki iliyopita na chini ni waombolezaji.
 Dansa wa zamani wa Pakistan  ambaye amekuwa akipigania maisha yake kufuatia shambulio la kumwagiwa tindikali lililoharibu kabisa sura yake, amejiua baada ya kuishi katika hali hiyo kwa miaka zaidi ya kumi.
Fakhra Younus mwenye miaka 33, amejiua wiki iliyopita kwa kujitupa kutoka jengo lenye ghorofa sita mjini Roma, Italia miaka 12 baada ya shambulio la kumwagiwa tindikali lililomfanya aonekane kama ‘sio binadamu’.
Wakati wa shambulio lake Mei, 2000, mume wake wa zamani Bilal Khar alikamatwa kwa tuhuma za kuingia kwenye nyumba na mama huyo na kummwagia tindikali Younus usoni wakati akiwa amelala.
Shambulio hilo lililotokea mbele ya mtoto wa Younus, ambaye wakati huo alikuwa na miaka mitano, limemwacha akiwa hawezi kupumua na hivyo kuishi kwa kuhesabu siku za kuishi.
Pua yake karibu yote iliyeyushwa na tindikali hiyo na amefanyiwa upasuaji mara 39 kujaribu kurekebisha sura yake kwa takribani miaka yote kumi iliyopita.
Tukio hilo la kutisha, limeunguza kabisa nywele zake, kuchoma midomo yake, kupofoa jicho lake moja, kuharibu sikio lake la kushoto na kuunguza matiti yake.
Baada ya kukimbizwa hospitali alisema, “Sura yangu ni gereza kwangu,” wakati mtoto wake naye akisema, “Huyu si mama yangu”.
Mama huyo alihamia Italia baada ya shambulio hilo ambako aliishi Roma na kuendelea na matibabu yake.
Lakini Machi, mwaka huu alijiua, baada ya kuacha ujumbe akisema anajiua kutokana na ukimya wa vyombo vya sheria katika kushughulikia suala lake kutojishughulisha kwa watawala wa Pakistan.
Bilal Khar alikamatwa mwaka 2002 na kushitakiwa kwa jaribio la kuua kufuatia shambulio hilo, kasha akaachiwa kwa dhamana miezi mitano baadaye. 
Khar, mbunge wa zamani na mtoto wa Gavana tajiri wa Pakistan, baadaye alifutiwa tuhuma za shambulio hilo, huku wengi wakiamini kuwa anawezekana ametumia nafasi ya familia yake kukwepa mkono wa sheria
Baada ya tukio la kushitusha la kujiua Younus, imeelezwa mapema mwezi huu kuwa, Khar ameendelea kukana kutia mkono kwenye shambulio la tindikali alipokuwa akihojiwa mtu tofauti mwenye jina lile lile akikanusha tuhuma.
Khar amedai mke wake huyo wa zamani amejiua sababu hakuwa na fedha za kutosha, si kwa sababu ya majeraha yake hayo ya kutisha.
Zaidi ya mashambulio 8,500 ya tindikali, ndoa za kulazimishwa na aina tofauti za unyanyasaji dhidi ya wanawake yameripotiwa nchini Pakistan mwaka 2011 kwa mujibu wa ripoti ya The Aurat Foundation, Taasisi ya Kupigania Haki za Wanawake.
Serikali ya Pakistani ilipitisha sheria dhidi ya mashabulio ya tindikali ambayo inaeleza kwamba yeyote atakayekutwa na hatia atatumikia kifungo kisichopungua miaka 14 jela.
Mke wa zamani wa baba yake Khar, Tehmina Durrani alijitolea kuwa wakili wa Younus na kusema kuwa mama huyo aliahidi kumfikisha aliyemshambulia kwenye vyombo vya sheria pindi atakapopata nafuu.
Durrani alisema: “Younus alinambia, “Nikirejea nitafufua kesi yangu, na nitapambana mwenyewe,” na hakika alikuwa mpambanaji.”
Durrani ametahadharisha kuwa kesi ya Younus iwe kumbukumbu kuwa serikali ya Pakistan inatakiwa iongeze nguvu zaidi kukomesha mashambulio haya ya tindikali na makosa mengine dhidi ya wanawake, na pia kuwasaidia waathirika wa mashambulio hayo.

No comments: