Waishauri serikali kufufua Nasaco

Jumuiya ya Mabaharia nchini (JMT), imeiomba serikali kufufua Shirika la Taifa la Wakala wa Meli Tanzania (Nasaco), ili kuwa na chombo cha kitaifa kitakachosimamia maslahi ya nchi kwenye sekta hiyo na kuondokana na ubadhirifu unaofanywa bandarini.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Frank Chuma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utayari wao wa kufanya kazi kwenye vyombo vya majini vya uchakataji, utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini.
Alisema ubadhirifu hauwezi kuisha bandarini kwa kuwa hakuna chombo cha kitaifa kinachosimamia meli zote zinazoingia na kutoka, hivyo inakuwa vigumu kwa taifa kuwa na takwimu halisi ya meli na idadi sahihi ya mizigo iliyobebwa na meli hizo.
“Bandarini kuna ubadhirifu mkubwa, na hauwezi kuisha iwapo Nasaco haitafufuliwa, hivi sasa kila meli ina wakala wake ambaye ndiye anayejua mzigo uliobebwa ni kiasi gani na wakati mwingine idadi ya uhakika haisemwi, lakini kama nchi ingekuwa na chombo cha kusimamia meli zote, ni wazi kwamba hakuna ubadhirifu ungetokea,” alisema Chuma.
Alisema taarifa za upotevu wa makontena bandarini unaotokea hivi sasa sio jambo la ajabu kwa sababu hakuna chombo cha kitaifa kinachokagua na kuhakiki idadi ya makontena yaliyoingia nchini, jambo ambalo wakati Nasaco ilipokuwa ikifanya kazi vitendo hivi vya upotevu wa makontena havikuwepo.
Chuma alisema serikali iangalie upya jinsi ya kufufua Nasaco kwa sababu ni chombo muhimu cha serikali kitakachodhibiti maslahi ya nchi na hivyo kuziba mianya ya ubadhirifu na hivyo nchi kuwa na takwimu sahihi za idadi ya meli na mizigo inayoingia na kutoka.
Akizungumzia utayari wa mabaharia wa Kitanzania kufanya kazi kwenye meli na vyombo vya utafutaji, uchimbaji, uzalishaji na usambazaji wa mafuta na gesi baharini, Chuma alisema wako tayari sasa kufanya kazi hizo baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria.
Alishukuru kwamba kilio cha muda mrefu cha mabaharia wa kizalendo kutopewa nafasi kufanya kazi kwenye meli na vyombo vya kutafuta mafuta na gesi, kimesikika.
“Sheria za vyombo vya meli ziko wazi, ila zilipindishwa tu na baadhi ya watendaji ambao kazi zinazopaswa kufanywa na mabaharia wa kizalendo pindi meli zinapotia nanga kwenye bandari ya Tanzania, zilifanywa na wageni, na sasa tumepigania hilo na tutahakikisha linatekelezwa,” alise

No comments: