Wadau kujadili nauli mabasi yaendayo haraka

Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) wiki ijayo inakutana na wadau kujadili nauli zitakazotumika kwa mabasi yaendayo kasi.
Kwa sasa kampuni ya UDA-RT inapendekeza nauli ya chini kuwa Sh  700 na wanafunzi kulipa nusu yake
Aidha, katika mapendekezo yake, UDA-RT inataka nauli ya safari kwenye njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1400 na wanafunzi nusu ya nauli hizo. 
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra ilisema maombi hayo kwa ajili ya kutoa huduma za mpito za usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika awamu ya kwanza ya mradi wa DART yatajadiliwa na wadau ili kuona uhalali wake.
Ilisema kwa mujibu wa sheria, Sumatra inapaswa kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kuridhia viwango  vya nauli.
“Katika kutekeleza hilo, mamlaka imeandaa mkutano ili kupokea maoni ya wadau ikiwa ni pamoja na watoa huduma, watumiaji wa huduma na wananchi kwa ujumla,” ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo wa wadau utafanyika Januari 5, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi ambapo wadau wote wa usafiri wanaalikwa.
Taarifa hiyo ilisema kabrasha lenye maombi ya nauli yaliyofanywa na UDA-RT linaweza kusomwa katika ofisi zao.

No comments: