Watu
wanane akiwemo Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi
la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Gerald Ryoba pamoja na familia yake, wamekufa maji baada ya gari walilokuwa
wakisafiria kusombwa na maji katika mkondo mpana wa mto unaotenganisha Kibaigwa
na Pandambili, mkoani Dodoma.
Watu sita
ni wa familia ya Ryoba waliokuwa ndani ya gari lililosombwa na maji
likijaribu kupita. Pia miili ya watu wengine wawili ambao pia walikufa kutokana
na kusombwa na maji, ilipatikana baada ya maji kuisha.
Pamoja
na msaidizi huyo wa IGP, wengine waliokuwa kwenye gari hilo lililosombwa na
maji, ni mkewe, Fidea Kiondo ambaye ni Mwalimu katika Manispaa ya Temeke,
jijini Dar es Salaam pamoja na watoto wao, Gabriel (4) na Godwin; msaidizi wa
kazi za ndani, Sarah na dereva, Koplo
Ramadhani.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David
Misime katika taarifa yake alisema kwamba Ryoba na familia yake walikuwa
wakitoka mkoani Geita kwenda Dar es Salaam.
Mtendaji
wa Kata ya Kibaigwa, Gabriel Mganga
alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba maiti wawili ambao ni tofauti na
waliokutwa kwenye gari, mmoja hakutambulika lakini mwingine amebainika ni Ofisa
Kilimo na Mifugo Kata ya Lenjulu,
wilayani Kongwa.
Mganga
alisema kwamba walilazimika kukata kwa gesi gari lililokuwa limebeba familia ya
msaidizi wa IGP baada ya kusombwa na maji kwa ajili ya kutoa watu waliokuwa
ndani. Wengine waliokotwa nje na kutambuliwa kutokana na vitambulisho
vilivyokutwa katika gari.
Alitaja
gari hilo ni aina ya RAV 4 yenye namba za usajili T 516 DEP.
Kwa
mujibu wa mtendaji huyo aliyekuwa kwenye eneo la tukio, dereva huyo wa polisi
alionywa asiingie katika mkondo huo
kutokana na wingi wa maji lakini hakuwasikiliza.
Alisema
baada ya kuingia kwenye mkondo, maji yaliitoa gari barabarani na kuitupa katika
korongo la mto kabla ya kwenda kusimama katika eneo lenye bwawa.
Alisema
mkondo huo ambao wengi hupaita Pasua, ni
moja ya sehemu korofi na madereva wengi hushitukizwa na maji kwa kuwa mkondo
huo unatoka mbali.
Diwani
wa Kata ya Kibaigwa, Kapinye
alisema eneo hilo linajulikana
kuwa korofi na ni pana na maji yake huja kwa kishindo.
Ilielezwa
kwamba maji hayo yaliyoanza kuingia barabarani juzi saa 11.30, yalisababisha magari zaidi ya 400
kukwama kila upande katika barabara hiyo kuu ya Dodoma-Morogoro.
Mafuriko
hayo ni matokeo ya mvua zilizonyesha katika Kata ya Njoge na Hembahemba wilayani Kiteto.
No comments:
Post a Comment