BUNGE LAWAHALALISHA MAWAZIRI WA MAGUFULI


Mawaziri walioteuliwa na kuapishwa na Rais John Magufuli kabla ya kula kiapo cha ubunge, wanaruhusiwa kushiriki shughuli za Bunge kama wabunge wateule.

Aidha, wateule hao wa rais hawalizuii Bunge kutekeleza wajibu wake wa kibunge kwa sababu kabla hawajaapa kiapo cha ubunge majukumu yao yanakuwa chini ya mawaziri waliokwishaapa bungeni ambao hukaimishwa na rais.
Ufafanuzi huo umetolewa jana na  Katibu wa  Bunge, Dk Thomas Kashilillah katika mahojiano yake na gazeti hili kufuatia uwepo wa maneno kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba kuna mgongano wa kikatiba kwa mawaziri walioteuliwa kuwa wabunge na rais kutekeleza wajibu wao kabla ya kula kiapo cha ubunge.
 Akifafanua hilo, Dk Kashilillah alisema shughuli zote za kibunge zinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Kanuni za Bunge, taratibu, mila na desturi za mabunge ya Jumuiya ya Madola.
Alisema kwa kuzingatia yote hayo, Bunge linaweza kuendelea na shughuli zake huku mawaziri ambao hawajala kiapo cha ubunge wakishiriki kama wabunge wateule na mwenendo wa shughuli hizo unatambulika kisheria na kikanuni kuwa ni halali.
Alisema wafuatiliaji wa mambo ya kibunge hawapaswi kuchanganywa na mijadala isiyo rasmi inayoendelea chini kwa chini kuhusu uhalali wa shughuli za Bunge, likiwa na baadhi ya mawaziri ambao hawajala kiapo cha ubunge.
Dk. Kashilillah alisema wanaotatizwa na jambo hilo wanapaswa kwanza kuelewa aina za wabunge wanaounda Bunge la Jamhuri ya Muungano na uhalali wa wabunge na waziri kutekeleza majukumu yao kabla ya kula kiapo.
“Ni vizuri kwanza kuelewa kuwa kuna wabunge wa majimbo,wabunge wanawake wasiopungua asilimia 30 ya idadi ya wabunge wa majimbo, wabunge watano toka baraza la wawakilishi, mwanasheria mkuu wa serikali, wabunge wa kuteuliwa na rais na Spika endapo siyo mbunge…
…“Pia ni vizuri ieleweke kuwa Ibara ya 76 ya Katiba inaeleza kuwa kuna uchaguzi wa wabunge kila baada ya Bunge kuvunjwa au inapotokea nafasi wazi wakati wowote baada ya Bunge kuzinduliwa kwa mara ya kwanza.
“Sasa mwaka 2015 uchaguzi ulifanyika Oktoba lakini kwa sababu mbalimbali majimbo matano hayakufanya uchaguzi hivyo idadi ya wabunge wanawake iliyotolewa ilikuwa pungufu lakini hivi sasa majimbo yote yamekamilisha uchaguzi na wabunge wamekwisha tangazwa. Hao wanasubiri kuapishwa ili washiriki shughuli za Bunge.
“Lakini uwepo wa wabunge ambao hawajaapishwa haulizuii Bunge wala kamati zake kutekeleza shughuli zake za kibunge, ila wabunge ambao hawajaapishwa hawataruhusiwa kuingia kwenye kamati  hizo hadi pale watakapoapishwa,ila sio kwamba kamati au bunge zima litasimamisha kazi zake,” alisema Dk. Kashilillah.
Alisema hivi sasa tayari Rais Magufuli amekwishateua wabunge sita kati ya kumi anaoruhusiwa kikatiba na kwamba tayari mmoja wa wateule wake aliyemteua kabla ya kuzinduliwa kwa Bunge la 11 amekula kiapo cha ubunge.
Dk. Kashilillah alisema wabunge watano wa majimbo ya Lushoto, Arusha Mjini, Handeni, Ludewa na Masasi na wabunge wanawake waliobaki pamoja na walioteuliwa na rais baada ya kuzinduliwa kwa Bunge wataapishwa kwanza Bunge litakapoanza kuketi Januari 26, 2016.
Aidha, katibu huyo wa Bunge alirejea uteuzi wa aliyekua Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo uliofanywa na Rais Mstaafu wa Awamu wa Nne, Jakaya Kikwete ambaye kabla ya kula kiapo cha ubunge alishiriki vikao vya Bunge kama mbunge mteule.
Alisema Prof Muhongo alishiriki shughuli za Bunge wakati nafasi yake ikishilikiwa na waziri mwingine ambaye rais alimteua kukaimu hadi alipoapishwa bungeni jambo ambalo linahusiwa kikanuni na kwamba utaratibu huo ndiyo utakaotumika mpaka hapo mawaziri walioteuliwa na Rais Magufuli watakapoapishwa bungeni.

No comments: