MAFURIKO YAKOSESHA MAKAZI KAYA 2,857

Kaya 2,857 wilayani Kilosa zimekosa makazi kutokana na nyumba 379 kubomoka na nyingine 997 kuzingirwa na maji yaliyotokana na mafuriko yaliyokumba wilaya hiyo ya Mkoa wa Morogoro.
 
Mafuriko hayo yametokana na mvua kubwa zilizonyesha katika safu za  milima ya  Wilaya za  Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma na  maji yake kujaa mto Mkondoa unaokatisha katika mji wa Kilosa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele alisema  hatua za awali ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuhifadhi kwa muda waathirika wa mafuriko kwenye  shule ya Msingi ya Lamlilo, mahakama ya mwanzo na katika ofisi ya mtendaji kata ya Magomeni.
Aidha alisema, mahitaji ya awali kwa waathirika hao yameshaandaliwa yakihusisha chakula, maji, dawa wakiwa eneo hilo kwa  muda wakisubiri kuhamishiwa katika  kambi maalumu zitakazotengwa.
Alitoa taarifa hiyo juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe aliyekwenda kukagua maeneo yaliyoathiriwa.
Henjewele alisema mafuriko hayo yalitokea usiku wa kuamkia Januari 5, pia yameathiri miundombinu ya barabara ya Kilosa – Mikumi  ambayo kwa sasa haipitiki.  Pia imeharibu mashamba  huku kata ya Magomeni ikitajwa kuathirika zaidi.
Pia nyumba 33 zilizopo katika  Kata ya Berega mapaa ya majengo ikiwemo vyoo vya shule za Msingi Kiegeya, Mugugu na Berega, yameezuliwa.
Diwani wa Kata  ya Magomeni, Abdallah Huwel  alishauri serikali kujenga  tuta upande wa pili wa mto Mkondoa. Kumbukumbu zinaonesha mafuriko makubwa yalitokea  mwaka 1964 na 1978, 1997;  Desemba 2009 na kuendelea hadi Januari, 2010 na kusababisha vifo vya watu wawili. Uliathiri watu 23,980  sawa na kaya  5, 605.

No comments: