Waziri
Mkuu Mizengo Pinda amesema Watanzania waishio ughaibuni hawataweza kupiga kura
wakiwa nje ya nchi kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, kwa sababu kuna mambo
kadhaa ambayo Serikali inabidi iyatekeleze kabla ya kufikiwa kwa hatua hiyo.
Aliyasema
hayo juzi wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Uingereza kwenye
makazi ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Balozi Peter Kallaghe, yaliyoko
Highgate, Kaskazini mwa Jiji la London.
Akizungumza
na Watanzania hao ambao baadhi yao walitoka miji ya Leicester na Manchester,
alisema mambo makuu ambayo yanahitaji kuzingatiwa kabla hawajaweza kupiga kura
ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 pamoja na
uandikishwaji wa Watanzania wana-Diaspora kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
"Najua
suala kubwa ambalo mnatamani kulisikia ni hili la Watanzania kuweza kupiga kura
kutokea huku mliko. Hili inawezekana lisifanikiwe wakati huu kwa sababu kuna
mambo muhimu ya kuzingatia kubwa likiwa ni marekebisho ya sheria na hili zoezi
la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura. Ili
mwananchi aweze kupiga kura ni lazima awe ameandikishwa kwenye Daftari la
Kudumu la Wapigakura.
"Itabidi
tuangalie kama mashine za BVR nazo zitapaswa kupelekwa kwenye kila ubalozi ili
watu wetu waweze kujiandikisha au itafutwe njia nyingine ya kufanikisha hilo
jambo.... lakini watu wa Tume wanaamini kwamba jambo hilo linaweza kufanikiwa
kwenye uchaguzi wa mwaka 2020," aliongeza.
Waziri
Mkuu ambaye aliwapatia nakala zisizopungua 40 za Katiba Inayopendekezwa,
alitumia fursa hiyo kuwasisitizia wasome kwa makini Katiba hiyo ili wawe na
uelewa mpana na kisha wailinganishe na Katiba ya mwaka 1977 ambayo inatumika
hivi sasa ili waweze kubaini kama kweli haina kitu kama ambavyo watu wengine
wanadai.
"Moja
ya changamoto zinazotukabili huko nyumbani ni mjadala kuhusu Katiba
Inayopendekezwa... wako watu wanaosema kwamba hakuna kitu kipya kabisa kwenye
Katiba Inayopendekezwa, lakini mimi nasema hayo ni mawazo yao binafsi,"
alisema.
Akifafanua
kuhusu Katiba hiyo, Waziri Mkuu alisema: "Mimi nilikuwa sehemu ya Bunge
Maalumu la Katiba, ni kweli tulibadili baadhi ya vipengele, lakini kwa nia ya
kuiboresha. Ninawasihi kila mmoja wenu aisome na kuangalia kama kweli hamna
kitu au kuna kitu kipya ikilinganishwa na Katiba inayotumika hivi sasa.
Angalieni na pimeni, je kuna kitu kimeboreshwa au la?"
Aliwasihi
waendelee kuiombea nchi ya Tanzania ili iendelee kuwa na amani na utulivu na
hasa katika kipindi hiki ambacho inakabiliwa na uchaguzi wa madiwani, wabunge
na Rais. "Ninawasihi muendelee kuiombea nchi yetu ili ipate viongozi
wazuri ambao watajali maslahi ya wengi," aliongeza.
No comments:
Post a Comment