Askofu Josephat
Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, amesema yeye si tajiri kama
inavyodhaniwa, bali alichonacho ikiwa ni pamoja na nyumba, magari na helikopta
ni baraka tu za Mungu, lakini kama ni utajiri, anatarajia siku moja utamshukia.
Aliyasema
hayo jana wakati akihubiri kanisani kwake Kawe, Dar es Salaam, ambako alisema
anawashangaa watu wanaomfuatilia maisha yake huku wakisema yeye ni tajiri
mkubwa.
“Wanaodai
mimi ni tajiri wana wivu tu na wananionea, mimi si tajiri, bali ni masikini
kama walivyo masikini wengine. Natarajia kutajirika hapo baadaye waumini wangu
wakiwa matajiri, siwezi kutajirika kama waumini wangu bado ni masikini,
nitatajirika pamoja nao,” alisema Gwajima.
Kuhusu
mgogoro unaoendelea baina yake na Jeshi la Polisi, Askofu Gwajima alisema yeye
anauona kama ni vita vya kiroho na hivyo ataendelea kumwomba Mungu ili amsaidie
kupambana na kilichopo mbele yake na anaamini kuwa atashinda vita hiyo kwa
uweza wa Mungu anayemtegemea.
“Mungu
wangu na awasamehe wote wanaonituhumu kuwa mimi ni tajiri na kuamua kudhoofisha
huduma, nasema huduma yangu haitakufa kamwe na wala hatutayumba katika mipango
yetu ya kuhubiri injili. Tutapigana kwa uweza wa Mungu na tutashinda kama
alivyosema kuwa tutapigana pamoja naye na tutashinda,” alisema Gwajima.
Akizungumzia
afya yake, Askofu Gwajima alisema kwa sasa anaendelea vizuri na anaweza
kusimama na kutembea, kuhubiri kama ilivyokuwa hapo awali na hatarajii kurejea
tena kwenye kiti cha baiskeli ya magurudumu matatu bali atasimama imara daima.
Kuhusu
kupeleka nyaraka kadhaa anazotakiwa aziwasilishe polisi siku ya mahojiano
Aprili 16, mwaka huu, Askofu Gwajima alisema suala hilo bado wanasheria wake
wanalishughulikia na wataendelea kufuata taratibu zote zinazotakiwa na jeshi
hilo.
Gwajima
anatakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu za hati ya usajili wa kanisa lake, namba
ya usajili wa kanisa, hati ya umiliki wa helikopta, hati ya nyumba anazomiliki,
idadi ya makanisa yaliyopo chini yake pamoja na hesabu za fedha za kanisani
kwake zinazohusu mapato na matumizi.
Nyaraka
zingine ni majina ya Bodi ya Udhamini wa kanisa, mpiga picha za video kanisani kwake siku ya ibada na shughuli
zingine za kanisani hapo pamoja na
waraka wa Maaskofu uliosomwa makanisani ambao Mwadhama Polycarp Kadinali
Pengo alioupinga na kusababisha yeye kumkashifu kiongozi mwenzake huyo wa dini.
Akionekana
kuwa makini sana na lugha anayotumia wakati wa kuhubiri, Gwajima aliwaomba
waumini wake waendelee kufuatilia kila sehemu na kuchunguza mambo yote mabaya
yanayosemwa juu yake na kanisa lake na kuyaripoti kwake au kwa uongozi wa
kanisa ili wayafanyie kazi mara moja kabla hayajaleta madhara.
“Nawaombeni
sana mfuatilie kila chanzo cha habari na kuchunguza mambo yote yanayosemwa juu
yangu au kuhusu kanisa na kuyaleta mara moja hapa kanisani ili tuyafanyie kazi
kabla hayajaleta madhara makubwa,” alisema Gwajima.
Aliongeza
kuwa, “tuendelee kuwa na umoja katika kipindi hiki ambapo shetani anataka
kupigana nasi ili tuweze kushinda. Tukifarakana hatutaweza bali tukiwa kitu
kimoja tutasonga mbele na kuwa huru”.
Wakati
akikana kuwa tajiri, mwanzoni mwa mwaka jana alifanya mahojiano na gazeti hili
na kukiri Mungu anambariki, ndiyo maana mambo yake yanamnyookea.
Aliyasema
hayo alipokuwa anazungumzia mpango wake wa kununua helikopta kwa ajili ya
huduma za injili ndani na nje ya nchi.
Alikiri
kutokana na utajiri anaosema unatokana na baraka za Mungu, anamiliki jumba la
ghorofa nne eneo la Mbezi Beach katika Manispaa ya Kinondoni. Pia amewanunulia
wachungaji wake 40 magari ya kutembelea kwa bei tofauti, yakiwemo ya chini ya
Sh milioni 10 na mengine ya zaidi ya Sh milioni 20.
“Ni
kweli nimewanunulia magari, unajua moja ya misingi yangu ya maisha ni kwamba,
mimi siwezi kuishi maisha mazuri, wakati wachungaji wangu wanadhalilika,
nimewanunulia magari karibia 40. Lakini nina wachungaji wa ngazi mbalimbali,
hawa ni wale wa juu, wengine wachungaji wadogo wapo zaidi ya 670, hawa ni
watenda kazi muhimu na wanatofautiana kwa ngazi zao, ndio maana kazi ya Mungu
inasonga mbele hata nisipokuwepo,” alisema Gwajima.
Mbali
na magari ya wachungaji, pia amenunua mabasi 20 ya kubeba waumini wake kutoka
na kwenda kanisani, yakianzia maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Alithibitisha kuwa, kila moja limegharimu kati ya Sh milioni 80 na Sh milioni
100.
Pamoja
na uwezo mkubwa wa kifedha alionao, Gwajima anayemiliki magari kadhaa likiwemo
la kifahari aina ya Hummer lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200, anasema kamwe hatageukia biashara kwa kuwa
hatafuti faida, bali kumtumikia Mungu ambaye naye anampa baraka za kipato
alichonacho kwa sasa.
No comments:
Post a Comment