TAARIFA KUHUSU RUBANI YAIBUA MAPYA NDEGE YA MISRI ILIYOANGUKA NA KUUA 66...


Utata kuhusu ajali ya ndege ya EgyptAir umeongezeka baada ya madai kwamba rubani wa ndege hiyo alitoa taarifa ya kuwapo moshi uliokuwa ukifuka kuashiria moto.

Ilidaiwa mwanzo Mohamed Said Ali Ali Shoukair alikosa mawasiliano yote ya radio kabla ya ndege hiyo aina ya Airbus A320 kuanguka baharini Alhamisi iliyopita, na kuua watu wote 66 waliokuwamo ndani yake, ikitokea Paris kwenda Cairo.
Lakini vyanzo vya habari za anga mjini Paris sasa vimesema aliwasiliana na waongoza ndege wa Misri kusema kwamba alikuwa akitarajia kutua kwa dharura sababu kuna moshi uliokuwa unatapakaa ndani ya ndege hiyo.
Kulikuwa na ‘majibizano yaliyodumu kwa dakika kadhaa’ kati Kapteni Shoukair na waongozaji ndege hao, ambayo yalipelekea ‘wito huo wa mashaka’, kwa mujibu wa televisheni ya Ufaransa ya M6.
Hatahivyo, madai hayo yalikanushwa na EgyptAir. Msemaji mmoja alisema: “Madai yaliyotolewa na televisheni ya Ufaransa si ya kweli. Rubani huyo hakuwasiliana na waongozaji ndege kabla ya ajali hiyo kutokea.”
Habari hizo zimekuja huku ndugu wa waliofariki kwenye ajali hiyo ya ndege iliyoanguka Alhamisi wakikusanyika pamoja kuomboleza kutokana na kuwapoteza wapendwa wao.
M6, chaneli ya televisheni ya Ufaransa, iliripoti kwamba rubani wa huyo akawasha kifaa maalumu cha ‘rapid descents’ kwa lengo la kuzima moto na kuondosha kabisa moshi huo uliokuwa umezagaa.
Rapid descents inahusisha mabadiliko makubwa kwenye mgandamizo wa hewa ndani ya chumba cha marubani, na inaweza kuwa hatari kubwa, lakini madai kuhusu matukio hayo ya mwisho ya ndege hiyo yanawiana na taarifa za awali.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Ugiriki, Pano Kammenos, ndege hiyo ilishuka kwa ghafla kutoka futi 37,000 hadi 15,000, na kisha ‘kwenda upande ghafla’.
Wakati ikiingia katika anga la Misri, maeneo ya kisiwa cha Karpathos kilichopo Ugiriki, mgeuko wa kwanza ulikuwa mkali, nyuzi 90 kuelekea Mashariki, na kisha kulikuwa na mzunguko kamili.
Ripoti hiyo iliyovuja pia inaelezea kwamba moto ulilipuka kwenye deki nzima ya ndege hiyo dakika kadhaa kabla ya janga hilo – ikieleza kushindwa kufanya kazi kwa vifaa vya umeme.
Taarifa hizo mpya zinaweka mbali ajali hiyo na uwezekano wa shambulio la kigaidi, ingawa bado uwezekani huo bado haujapuuzwa hilo.
Rais wa Misri, Abdel-Fattah el-Sisi amevunja ukimya kuhusu ajali hiyo ya ndege, akisema nyambizi zitatumika kusaka kisanduku cheusi cha ndege hiyo na virekodia sauti, ambavo huhifadhi mawasiliano kwa mwzi mmoja tu kabla ya betri kuisha nguvu.
Alisema ‘yote hayo yanawezekana’.

No comments: