Watu 18
wamekufa papo hapo kwa kuteketea kwa moto na wengine 11 wamejeruhiwa vibaya
kutokana na basi walilokuwa wakisafiria
kugongana na lori aina ya Mitsubishi Fuso, katika kijiji cha Msimba tarafa ya
Mikumi, barabara kuu ya Morogoro –
Mbeya.
Ajali
hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Nganga linalofanya safari zake kutoka Wilaya
ya Kilombero kuelekea mkoani Mbeya na kugongana na lori hilo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alisema ajali hiyo ilitokea jana saa
mbili asubuhi katika eneo hilo huku likihusisha basi aina ya Scania lenye namba
za usajili T373 DAH na Fuso lenye namba za usajili T164 BKG.
Alisema
chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi la Nganga ambaye alikuwa katika mwendo
kasi na kulipita gari lililokuwa mbele yake bila ya tahadhari na kukutana na
lori hilo na kisha kugongana nalo katika eneo hilo.
Alisema
baada ya magari hayo kugongana, ndani ya buti ya basi kulikuwa kumepakiwa
pikipiki ambayo ilikuwa na mafuta na baada ya kutokea ajali hiyo kulitokea
mlipuko wa moto na kusababisha basi hilo pamoja na lori kuwaka moto.
Kamanda
huyo alisema kuwa kutokana na moto huo, baadhi ya abiria waliokuwepo katika
basi hilo walishindwa kujiokoa na hivyo miili yao kuteketea kabisa na moto huo,
wakiwemo madereva wote wa magari hayo.
Alisema
majeruhi 11 wa ajali hiyo wamekimbizwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito
iliyopo tarafa ya hiyo Mikumi kupatiwa matibabu huku hali zao akieleza kuwa
baadhi yao ni mbaya kutokana na kuungua vibaya kwa moto.
Kamanda
huyo alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali hiyo ambapo
mpaka sasa haijatambulika majina yake, licha ya madereva wa magari yote kufa.
Hata
hivyo, Kamanda huyo alishindwa kutaja majina ya majeruhi kutokana na baadhi yao
kuendelea kupatiwa matibabu kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Naye
Mganga wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito
iliyopo Mikumi, Dk Boniventure
Buyagabuyaga,
alithibitisha kupokea jumla ya miili ya marehemu 18 ambao walikuwa wameteketea
vibaya kwa moto kutokana na ajali, ambapo alisema tayari imehifadhiwa katika chumba cha
kuhifadhiwa maiti kwa ajili ya kusubiri utambuzi.
Alisema
mpaka sasa majeruhi wanaotibiwa katika hospitali yake wamebaki saba, lakini
hali zao bado ni mbaya kutokana na kuungua moto katika sehemu mbalimbali za
miili yao.
Ajali
hiyo imekuwa sawa na mwendelezo wa ajali za mabasi nchini, kwani Alhamisi
iliyopita watu 12 walikufa katika ajali zilizotokea Tanga na Morogoro, huku
wengine wanne waliokuwa wakisafiri kwa basi la Nyehunge wakiaga dunia usiku wa
Jumamosi mkoani Dodoma.
Katika
ajali iliyotokea mkoani Tanga, katika kijiji cha Mbweni Mkata, majira ya
asubuhi, ilihusisha basi la Kampuni ya Ratco ya Tanga liligongana uso kwa uso
na basi la kampuni ya Ngorika na gari dogo aina ya Toyota Passo na kusababisha
vifo vya watu 10 papo hapo, akiwemo mmiliki wa gari dogo, Musa Lupatu aliyekuwa
Mbunge wa zamani wa Korogwe Vijijini.
Katika
tukio la Morogoro, watu wawili walikufa na wengine 48 kujeruhiwa katika ajali
iliyosababishwa na basi la Happy Nation lililokuwa likitoka Dar es Salaam
kwenda Mbeya na kupata ajali eneo la Mikumi.
Aidha,
Machi 12, mwaka huu mkoani Iringa, basi la Majinja Express lilikuwa likitokea Mbeya kwenda Dar
es Salaam liligongana na lori na kisha
likaangukiwa na kontena lililosababisha vifo vya watu 43.
No comments:
Post a Comment