KURA YA MAONI YAAHIRISHWA HADI DAFTARI LA WAPIGAKURA LIKAMILIKE


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesogeza mbele kwa muda usiojulikana shughuli ya upigaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.

Awali, Watanzania walikuwa waipigie kura Katiba hiyo Aprili 30, mwaka huu.
Lakini jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema hatua hiyo imetokana na kutokamilika kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Kwa vile kazi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura ni ya msingi kabla ya kupiga kura, na jukumu la kwanza la Tume ni kukamilisha kazi ya kuboresha daftari. Mengine yanafuata baada ya hapo,”alisema.
Aliongeza: “ Kwa vile zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijakamilika, Tume haitaweza kuendelea na zoezi la kupiga kura ya maoni kama ilivyotangazwa awali.”
Awali, ilitangazwa baada ya kukamilika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo mpya wa BVR nchini nzima, upigaji kura ungefanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Tume ilianza Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa Biometrick Voters Registration (BVR) baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe, Februari 24 mwaka huu.
Alisema muda mwafaka ukifika, Tume itatangaza tarehe mpya ya Kupiga Kura ya Maoni baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Akizungumzia vifaa, Jaji Lubuva alisema kuwa serikali imeshalipa dola za Marekani milioni 72 (sawa na Sh bilioni 122.4) kwa ajili ya vifaa hivyo na kuwa vifaa 7,750 vilivyosalia, vitaletwa nchini kwa awamu.
Katika mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu  la Wapiga Kura kwa mfumo mpya wa BVR, Tume ilihitaji vifaa 8,000 na ilianza na vifaa 250
“Nikiri kulikuwepo na ucheleweshaji wa kulipia vifaa vya kuandikisha wapiga kura, lakini sasa Serikali imelipia vyote, na vitaletwa kutoka China kwa awamu, siku chache zijazo tutapokea vifaa 248 na baadaye vifaa 1,600 na vitafika kwa awamu mpaka idadi itakapofikiwa,” alisema.
Alisema kutokana na kuanza kuingia kwa vifaa hivyo, Tume imejipanga kuhakikisha inakamilisha Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ukamilifu ifikapo Julai mwaka huu.
Aidha, Lubuva alisema kazi ya uandikishaji wapigakura kwa mkoa wa Njombe, unatarajia kukamilika Aprili 18 mwaka huu na kuwa baada ya hapo Tume itakwenda Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mtwara na Lindi.
“Kama ilivyokuwa Njombe, Tume inatarajia mikoa inayofuata itawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao na kujiandikisha kwa tarehe zitakazotangazwa kwenye mikoa husika,”
Hata hivyo, Lubuva alisema kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wadau, wanaoona kuwapo kwa foleni ndefu kuwa ni dalili ya ubovu wa mfumo wa BVR, lakini ukweli hali hiyo ndiyo kielelezo cha kukua na kukolea kwa demokrasia nchini.
Licha ya makundi kadhaa kujaribu kuipinga Katiba hiyo Inayopendekezwa, wakiwemo baadhi ya viongozi wa dini na vyama vya siasa vya upinzani, imeelezwa kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wataipigia Kura ya Ndiyo Katiba Inayopendekezwa.
Aidha, imeelezwa mwito wa vyama vinavyounda umoja wa Ukawa wa kususa kura ya maoni haujawavutia wananchi wengi, hivyo wengi hawauungi mkono.
Hayo yamo katika taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza kati ya Januari 27 na Februari 17 mwaka huu na kutolewa jana kupitia muhtasari wenye jina la “Kuelekea Kura ya Maoni ya Watanzania kuhusu Katiba Inayopendekezwa.”
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo uliosambazwa kwa vyombo vya habari na Mshauri wa Mawasiliano wa Twaweza, Risha Chande, muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi.
Muhtasari huu unajumuisha maoni ya wananchi wa Tanzania Bara pekee juu ya Katiba Inayopendekezwa.
“Jumla ya wahojiwa 1,399 walipigiwa simu kati ya Januari 27 na Februari 17, 2015. Matokeo mengine yanatokana na duru la 5 la Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,708 kati ya Julai 16 na Julai 30, 2013) na duru la 14 la Sauti za Wananchi  (iliyowahoji watu 1,550 kati ya Februari 12 na Machi 4, 2014).
Kuhusu Ukawa kususa vikao vya Bunge la Katiba na ushawishi wake kwa wananchi kususa kura ya maoni, utafiti huo umeonesha: “Kati ya wananchi waliosikia minong’ono juu ya Ukawa kususa vikao vya Bunge la Katiba, asilimia 66 wanapinga hatua hiyo. Asilimia 68 wanapinga ushawishi kwa wananchi kususa kura ya maoni na robo tatu (asilimia 75) ya wananchi wanasema hawatasusa kura ya maoni.”

No comments: