MWALIMU WA MADRASA ANASWA NA WATOTO 11


Mwalimu wa Madrasa, Alhaji Maulana Shiraz (71) wa Jumuiya za Wi’yatu LiQadria iliyoko kijiji cha Chikundi wilayani Masasi mkoa wa Mtwara, anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilaya ya Masasi kwa tuhuma za kukutwa na watoto wadogo wapatao 11, wa kike na wa kiume, kinyume na taratibu na sheria za nchi.
Pia, amekutwa na fomu za usajili zinazoonesha taarifa muhimu za mwanafunzi hao, zikiwemo jina la mtoto, jina la mzazi, mahali anakotoka kwa maana ya kijiji na kata pamoja na mawasiliano ya mzazi au mlezi wa mwanafunzi.
Watoto waliokutwa katika kituo hicho ambao wanatoka katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Lindi na Mtwara ni Selemani Juma (12) wa kijiji cha Mandawa, Ruangwa,  Bakari Nang’ani (12) anayetoka pia Ruangwa, Jamal Abbas (12) na Mwajuma Selemani (12) wanaotoka Mwena, Masasi, Karim Abbas (17) mkazi wa Liwale mkoani Lindi.

Wengine ni Mark Muhidin (12), Haji Juma (18), Ganafi Hamisi (13) na Murji Muhidin (12), wakazi wa kijiji cha Mkululu wilayani Masasi, Nurdin Ausi (11) kutoka kijiji cha Mpanyani, Masasi na Ally Bakari (12) mkazi wa kijiji cha Milola mkoani Lindi. Pia yumo Hamis Seif (05) mkazi wa kijiji cha Kanyimbi wilayani Masasi katika mkoa wa Mtwara.
Jeshi la Polisi wilayani Masasi limethibitisha tukio hilo kupitia kwa Kaimu Mkuu wa jeshi hilo wilaya ya Masasi, Nathanael Kyando na kusema linamshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi ili kubaini alikuwa na nia gani juu ya watoto hao.
Akizungumza na mwandishi, Alhaji Maulana alikiri kukaa na watoto hao walioletwa na wazazi na walezi wao kwa zaidi ya miezi miwili nyumbani hapo kwa  madai ya kuwapa elimu ya dini ya Kiislamu kwa muda wa miaka mitatu ili aweze kupata thawabu kutoka kwa Mungu.
Alisema hakuwa na nia mbaya ya kukaa na watoto hao, ingawa amekiri kufanya makosa ya kukaa na watoto ambao walistahili kuwepo shuleni kupata elimu dunia.
Aliomba Jeshi la Polisi limwachie huru, kwa kuwa alichokitenda ni moja ya ahadi ambayo aliiahidi kuwa ataitimiza mara tu baada ya kurejea kutoka kwenye “Ibada ya Hijja” mwaka 2013.
Alhaj Maulana alisema alianza kukaa na watoto hao Desemba mwaka jana kwa makubaliano na wazazi wao kuwa masomo chuoni hapo, yataanza rasmi Januari 30, 2015 huku moja ya sharti la chuo likiwa ni mzazi kugharimia matibabu ya mtoto wake pindi atakapolazwa.
Katika hali ya kushangaza ni pale Katibu Tawala wa Wilaya ya Masasi, Danford Peter alipoamua kupiga moja ya namba ya simu ya mzazi wa mtoto, Ally Bakari (0783-812523) anayetoka kijiji cha Milola, Lindi aliyefahamika kwa jina la Bakari Mtapila.
Mtu huyo alipopokea simu, alikana kuwa jina hilo si lake na hana mtoto mwenye jina hilo anayeishi Masasi, licha ya kukiri kuwa ni mkazi wa Milola.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Bernard Nduta, aliyekuwepo eneo la tukio, alisema wao kama serikali wameviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo na hatimaye watatoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari.
Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Thabit Thabit alisema mzee huyo ametenda kosa la kukaa na watoto hao, ambao amewakosesha haki zao za msingi ikiwemo elimu.
Alikiri kuwa hata mazingira ambayo watoto hao wanaishi si mazuri, kwani walikuwa wakilala zaidi ya watoto wanne katika chumba kimoja na mbaya zaidi walikuwa wanalala chini ya sakafu, iliyotandikwa vipande vidogo vya magodoro.

No comments: