GWAJIMA KUHOJIWA TENA POLISI WIKI IJAYO


Mahojiano baina ya Jeshi la Polisi na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima yaliyokuwa yanatarajiwa kuendelea jana, ikiwa ni siku mbili baada ya kuachiwa kwa dhamana na jeshi hilo, jana yalikwama kuendelea kutokana na kile kilichoelezwa kutoimarika kwa afya ya askofu huyo, na sasa yatafanyika Alhamisi ijayo.

Gwajima alidaiwa kuzimia wakati akihojiwa na makachero wa Polisi waliokuwa wanamhoji, alipojisalimisha alasiri ya Ijumaa iliyopita baada ya kutakiwa kufanya hivyo, kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
Kutokana na hali hiyo iliyotokea majira ya saa tatu usiku wakati akiendelea na mahojiano yaliyoanzia alasiri, alikimbizwa Hospitali ya TMJ, Mikocheni akiwa chini ya ulinzi wa Polisi hadi aliporuhusiwa kutoka Jumanne wiki hii na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Mwanasheria wa Askofu Gwajima, John Mallya alithibitisha kuahirishwa kwa mahojiano kati ya mteja wake na Polisi, akisema mapema jana asubuhi aliripoti Kikuo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kama alivyotakiwa kuripoti kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.
Hata hivyo, alisema hakuweza kuhojiwa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa afya ya mteja wake haijaimarika vizuri na hivyo wamepangiwa kurudi tena kituoni hapo Aprili 9 mwaka huu, yaani Alhamisi ijayo kwa ajili ya mahojiano.
“Mteja wangu alifika kituoni leo (jana) asubuhi kwa ajili ya mahojiano na pia kuripoti kama ilivyoagizwa siku alipopatiwa dhamana, hata hivyo afya yake bado haijaimarika na hivyo imewalazimu polisi wampatie muda zaidi hadi Aprili 9 atakaporudi tena kwa ajili ya mahojiano,” alisema Mallya.
Hata hivyo, Mallya alisema hali ya afya ya Gwajima imeanza kuimarika na kadri siku zinavyozidi kwenda, atakuwa na nguvu na ataendelea na kazi zake kama kawaida.
Mtumishi huyo alipatiwa dhamana katika Kituo cha Polisi Oysterbay na kutakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Kati kwa ajili ya mahojiano zaidi na kusubiri uchunguzi wa kesi yake ukamilike.
Akiwa hospitalini TMJ, wafuasi wake 15 wakiwemo wachungaji sita, mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa kile kilichoelezwa kula njama za kutaka kumtorosha askofu huyo bilionea anayemiliki utitiri wa magari likiwemo aina ya Hummer lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 250, nyumba ya ghorofa ya kifahari, helikopta na kadhalika.
Kukamatwa kwa wafuasi hao ambao nao wamefunguliwa mashitaka, kulithibitishwa na Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Katika taarifa yake, alisema watu hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama pamoja na kujaribu kumtorosha Askofu Gwajima aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya TMJ kwa matibabu.
Alisema siku ya tukio (usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita), saa tisa na nusu usiku, watu 15 walifika hospitalini hapo kwa lengo la kumuona mgonjwa huyo.
“Askari ambao wapo katika lindo hilo waliwatilia mashaka watu hao hivyo waliwakatalia kuingia. Na hapo walijaribu kutumia nguvu, lakini walikamatwa,” alisema.
Kova alisema baada ya kuwapekua, watu hao walikutwa na bengi lenye bastola aina ya BERRETA yenye namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za Short gun na vitabu viwili vya hundi.
Alisema begi hilo pia lilikuwa na hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Joseph Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundi cha Benki ya Equity, nyaraka mbalimbali za kampuni ya PUMA, chaja ya simu na tablets, suti mbili na nguo za ndani.
Aliwataja waliokamatwa ni Chitama Mwakibambo (32), fundi seremala mkazi wa Gongo la Mboto, mchungaji Edwin Audex (24) mkazi wa Kawe Maringo, Adam Mwaselele(29), mhandisi na mkazi wa Kawe Maringo, Frederick Fusi (25) mkazi wa Mbezi Beach.
Wengine mwanafunzi wa chuo cha IMTU, Frank Minja (24) mkazi wa Mbezi Beach, Emmanuel Ngwela (28) mkazi wa Keko Juu ambaye ni mlinzi shirikishi, Geofrey William (30), Mhadhiri UDSM mkazi wa Survey Chuo Kikuu, Mchungaji Mathew Nyangusi (62) mkazi wa Mtoni Kijichi, Mchungaji Boniface Nyakyoma (30) mkazi wa Kitunda.
Pia wametajwa Geofrey Andrew (31), dereva mkazi wa Kimara Baruti, Mchungaji David Mgongolo (24) mkazi wa Ubungo Makoka, Mfanyabiashara George Msava (45) mkazi wa Ilala Boma, Mchungaji Nicholaus Patrick (60) mkazi wa Mbagala Mission, George Kiwia (37) ambaye ni dalali wa magari na mkazi wa Tandale Uzuri na Mchungaji Yekonia Bihagaze (39) mkazi wa Kimara Stop Over.
Kova alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa madhumuni ya kubaini sababu za njama hizo sambamba na kujua mbinu zote zilizotumika kutaka kufanikisha jaribio la kumtorosha Askofu Gwajima.

No comments: