BEI ZA VYAKULA ZAPAA KARIAKOO KUELEKEA PASAKA


Bei za mazao katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu  za Pasaka katika soko la Kariakoo zimeongezeka kutokana na imani iliyojengeka kwa wafanya biashara kuwa uwezo wa manunuzi unakuwa juu.

Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Florens Seiya alisema jana katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
Seiya alisema kila inapofikia kipindi cha sikukuu kubwa za kidini, imekuwepo desturi kwa wafanyabiashara nchini kupandisha bei za vitu sio kwenye bidhaa tu hata nguo ama usafiri.
Alitaja bidhaa zinazopanda bei katika kipindi hiki kuwa ni nyanya maji, vitunguu maji, pilipili hoho, vitunguu swaumu, tangawizi, karoti, njegere, matunda mbalimbali na mchele. Alisema wastani wa ongezeko za bei hizo ni Sh 5,000 hadi 100,000 kutokana na aina ya  mazao.
Alitolea mfano nyanya kwa kawaida hivi sasa boksi ni Sh 35,000 lakini kipindi hiki imekuwa Sh 40,000. Mchele gunia ni Sh 150,000 kipindi cha sikukuu ni Sh 200,000. Tangawizi awali gunia liliuzwa Sh 200,000 hivi sasa ni Sh 300,000.

No comments: