MWENYEKITI WA WAFANYABIASHARA AACHIWA KWA DHAMANA


Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mjini jana ilimwachia kwa dhamana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja (34), huku taarifa kutoka mikoa mbalimbali zikisema wafanyabiashara nao wamelegeza mgomo wao na kufungua maduka.

Minja (pichani) alifutiwa dhamana kwa kile kilichodaiwa kuendelea kuhamasisha wafanyabiashara wasilipe kodi kwa serikali wakati akiwa nje kwa dhamana.
Kuachiwa kwa mtuhumiwa huyo kulizusha shangwe kwa mamia ya wafanyabiashara  kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao walifurika mahakamani hapo kusikiliza kesi ya kiongozi wao huku ulinzi ukiwa umeimarishwa .
Kutokana na mwenyekiti huyo kuachiwa idadi kubwa ya wafanyabiashara ambao walizuiwa kwenye lango kuu la kuingia mahakamani walitawanywa na polisi huku wengine wakikataa kuondoka mpaka wamuone Minja huku wakili upande wa utetezi Godfrey Wasonga akiwatangazia mara kwa mara wananchi hao kuondoka eneo la mahakama kwani mwenyekiti huyo hatazungumza chochote na wafanyabiashara.
Uamuzi wa kumuachia kwa dhamana Minja ulitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Rhoda Ngimilanga baada ya kusikiliza hoja za upande wa mashtaka na upande wa utetezi.
Wakili wa Serikali, Rose Shio alisema mara ya mwisho mshtakiwa alifutiwa dhamana kwa sababu ya kukiuka masharti aliyowekewa na mahakama Januari 28, mwaka huu, wakati alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kushtakiwa kwa mashtaka ya kuwashawishi wafanyabiashara kugomea kutumia mashine za EFDs na wasilipe kodi kwa serikali.
Alidai wanakubali dhamana ni haki ya mshtakiwa lakini inatakiwa kwenda pamoja na masharti kwani kulikuwa na taarifa kwenye hoteli aliyofikia aliitisha mkutano na ajenda zilizokuwa zikijadiliwa ni mgomo wa matumizi wa mashine za EFD’s.
“Ilikuwa ni sahihi kwa Minja kufutiwa dhamana” alidai wakili wa serikali
Akijibu hoja hiyo, Wakili upande wa utetezi, Godfrey Wasonga alisema anapinga hoja za wakili wa serikali kwani dhamana ni haki ya mshtakiwa kikatiba kwani inatoa haki ya mtu kupata dhamana  ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa kuendelea kumuweka rumande Minja ni kama tayari ameshatiwa hatiani wakati mahakama bado haijaamua kama ana hatia au la.
“Tukimwachia Minja aendelee kukaa Isanga tutakuwa tumevuruga katiba ambayo ni sheria mama kwani hajawahi kuvunja masharti ya dhamana” alisema
Alidai Minja hakuwahi kufanya mkutano na mahakama isiendelee kusikiliza umbea kutoka kwa wakili wa serikali, kwani kama aliitisha mkutano angekamatwa na kufikishwa kunakohusika na si mahakama kuamini maelezo ya upande wa mashtaka ambayo hayana ushahidi wowote.
Akitoa uamuzi wa mahakama, hakimu Ngimilanga alisema amesikiliza maelezo ya pande zote mbili na kitu kikubwa upande wa mashtaka unadai mshtakiwa alivunja masharti ya dhamana kwa kufanya mkutano na kusababisha kuvunjika kwa amani.
Kutokana na hilo hakimu Ngimilanga alisema mshitakiwa atakuwa nje kwa dhamana hadi Aprili  9, mwaka huu kesi yake itakapoanza kusikilizwa maelezo ya awali.
Jijini Dar es Salaam, hali katika maduka ya Kariakoo yalirejea katika hali ya kawaida, kwani yalifunguliwa nyakati za mchana baada ya mahakama kumwachia kwa dhamana Minja. Hali kama hiyo iliripotiwa kutokea katika mikoa mbalimbali nchini.

No comments: