Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, juzi alichangia kuyaokoa maisha ya
Amina Bakari (20), mjamzito aliyesota porini kwa saa sita akisubiri usafiri wa
kumfikisha hospitali ya wilaya iliyopo Utete kwenda kujifungua.
Kabla ya msaada wa mbunge huyo
aliyekuwa katika ziara jimboni kwake, Amina alikodi pikipiki imwahishe
hospitali, lakini baada ya umbali fulani, mama huyo alishindwa kuhimili
mtikisiko na kuomba ashushwe kwa kuwa pia dalili za uchungu wa kujifungua zilikuwa
zimeongezeka.
Dereva wa bodaboda, Mussa Idd alisema
aliridhia kumsikiliza mteja wake na hivyo kumshusha katika eneo la Nyagolombe
mpakani mwa kijiji cha Utungi na Nyamwage, lakini kwa zaidi ya saa sita mama
huyo hakupata usafiri, huku akihangaika kutokana na kushikwa na uchungu.
“Lakini tukiwa tumeshakata tamaa na kusubiri
ajifungue tukiwa porini, lilitokea gari na nikasimamisha ili kuomba msaada.
Kumbe lilikuwa na mbunge wetu, hakuwa na hiyana alitusaidia kumkimbiza mgonjwa
hospitalini umbali wa kilometa 20…,” alisema.
Akiwa katika ziara hiyo, Dk Rashid
aliyezungukia vijiji na miradi mbalimbali, aliwataka wananchi wa Jimbo la
Rufiji kuthamini michango inayotolewa kwa ajili ya kuimarisha afya, umeme,
shule na uboreshaji wa sekta ya mawasiliano katika wilaya ya Rufiji.
Akizungumza juzi na watendaji wa
Serikali za Mitaa ngazi ya vitongoji katika kijiji cha Garambe, Dk Rashid alisema mambo
yaliyofanyika katika wilaya hiyo ni
mengi na yenye tija kwa kila mwananchi, hivyo waiheshimu michango hiyo kwa kuigeuza
kuwa fursa za maendeleo.
Alisema wilaya ya Rufiji inaongoza
kwa kuwa na magari ya kubebea wagonjwa kuliko
nyingine hapa nchini, pia wilayani humo kumejengwa kituo cha afya karibu kila
kata pamoja na zahanati,kitu ambacho ni cha kujivunia katika uongozi wake.
"Hadi sasa wilaya ina magari
saba ya kubebea na huenda yakaongezeka kutokana na kuendelea kuwashawishi
wafadhili wa ndani na nje ili kusaidia
hilo, pia acheni kurubuniwa na watu wachache wanaosema kuwa sijafanya
chochote hapa jimboni," alisema.
Alisema katika kituo cha Afya
Ikwiriri, kipo chumba cha upasuaji
kinamaliziwa kujengwa kwa gharama ya Sh milioni 150 ambacho kitakuwa cha
kisasa na kitasaidia wakazi wa wilaya hiyo
pamoja na za jirani.
No comments:
Post a Comment