APAMBANA NA MAMBA KWA ZAIDI YA NUSU SAA MKOANI RUKWA


Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Udasi mwambao mwa Ziwa Tanganyika, kata ya Kabwe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Ismail Ndomboya (42) amenusurika kuuawa na mamba kwa kupambana kijasiri na mnyama huyo kwa  zaidi ya nusu saa.

Hata hivyo, licha ya  kuokoa  maisha yake  mnyama huyo katika mapambano hayo  alimng’ata   na kumnyofoa  mkono wake wa kulia na  kutokomea  nao  ziwani.
Diwani wa Kata ya Kabwe, Asante Lugwisha  akizungumza na mwandishi wa  habari hizi  kwa  njia ya simu alithibitisha kutokea kwa mkasa huo  uliotokea  juzi  saa moja na nusu  jioni  wakati Ismail  alipokuwa akioga  katika Ziwa Tanganyika  kijijini Kabwe .
Akisimulia  mkasa  huo, Diwani  Lugwisha  alibainisha kuwa  jioni  hiyo ya tukio Ismail  aliamua  kwenda  kuoga  ziwani  wakati huo akiwa pekee  ndipo  ghafla  mamba alimvamia ghfla na  kumuuma mkono wake wa kulia.
“Kwa ujasiri mkubwa Ismail alipambana  kufa au kupona na mnyama  huyo  kwa  nusu saa  huku akipiga yowe akiomba  msaada  lakini  hakuna  aliyejitokeza kumsaidia  kwa  sababu sehemu aliyokuwa akioga  ilikuwa mbali na makazi  ya watu,“ alieleza.
Aliendelea  kueleza kuwa  hatimaye  mamba  aliunyofoa  mkono wa kushoto wa Ismail na kutokomea  nao  ziwani  ndipo  Ismail  alipokimbia  kuelekea  nyumbani kwake  akiwa  uchi.
“Baadaye nilitaarifiwa kuwa Ismail ameshambuliwa na  mamba  wakati akioga  ndipo  nilipofika nyumbani kwake, na tulijipanga tukamkimbiza  katika Hospitali Teule ya Wilaya (DDH) mjini  Namanyere ambao  tulifika saa  nne na nusu  usiku  ambako  amelazwa kwa matibabu “  alieleza.
Mtaalamu wa afya  wa Hospitali ya  Wilaya, ambaye  alikiri kuwa si  msemaji,  alikiri  kupokelewa kwa mgonjwa  huyo  aliyejeruhiwa  na mamba  ambapo  aliielezea hali yake  kuwa inaendelea vizuri. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda  amethibitisha kutokea kwa mkasa huo  na kwamba  uchunguzi wa  tukio hilo  unaendelea.

No comments: