Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam
imetupilia mbali ombi la kuitaka kampuni ya uwekezaji ya VIP Engineering and
Marketing, kutoa majibu ya ziada kwa maswali ya awali katika kesi ya Sh bilioni
787 inayohusu kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL).
Jaji Salvatory Bongole alitoa uamuzi
huo dhidi ya ombi lililowasilishwa na
kundi la mabenki linaloundwa na Standard Chartered Bank PLC, Standard
Chartered Bank (Hong Kong)Limited, na ya Tanzania Limited pamoja na wafilisi wa
Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad.
Akitoa uamuzi huo Jaji Bongole
alisema amri iliyotolewa Januari 27,
mwaka huu na Mahakama hiyo kuhusu wahusika wengine katika kesi hiyo, Wartsila
NederlandBV na Wartsila Tanzania Limited, ambao pia walidai kupewa majibu ya
maswali hayo ya ziada, pia inazihusu benki hizo pamoja na wafilisi wa
MechmarCorporation.
Katika amri hiyo, Jaji Bongole
alisema hawezi kuruhusu utoaji wa majibu zaidi kwa sababu haitakuwa kwenye
mazingira ya kutenda haki katika kutoa uamuzi wa shauri hilo au kusaidia
kupunguza gharama.
Jaji Bongole alisema baada ya
kuzingatia ombi la walalamikiwa na kiapo cha pingamizi kwenye majibu hayo,
aligundua kuruhusu majibu zaidi katika hatua hiyo ya shauri kutasababisha
kuivuruga kesi hiyo jambo ambalo haliruhusiwi kisheria.
Alisema kwa hatua hiyo kampuni ya VIP
Engineeringand Marketing imewasilisha nyaraka zake za majibu kwa njia ya
maandishi hivyo wamekamilisha nyaraka zote zinazohitajika na zile ambazo
ziliombwa lakini hazijaletwa zitaombwa wakati wa kuhojiana kesi itapokuwa
inaendelea.
Awali wakati wa usikilizwaji wa ombi
hilo, Wakili wa kampuni ya VIP, Michael Ngalo, alidai kuwa ombi hilo kuhusu
kupewa nyaraka zaidi halina msingi, ni ya kashfa na yenye kuwakandamiza na pia
yameletwa bila ya kufuata taratibu za kimahakama.
Wakili Gasper Nyika, kwa niaba ya Kundi
la Benki, alidai katika kiapo kinachounga mkono ombi hilo kuwa, kampuni ya VIP
haijatoa vielelezo vya kutosha kama ilivyoamriwa na majibu yaliyotolewa
hayakutosheleza.
Hata hivyo, Wakili Ngalo alidai
wametoa majibu yanayotosha kwa maswali hayo hasa kama Standard Chartered ni
mwezeshaji wa kifedha wa IPTL ambapo wamejibu kwa sasa hakuna muwezeshaji wa
aina hiyo na pia benki ya Standard Charetered siyo mkopeshaji wa IPTL.
Katika shauri la msingi, kampuni ya
VIP imefungua mashitaka dhidi ya walalamikiwa kwa kula njama za pamoja na
kuhujumu maslahi yake katika kampuni ya IPTL aidha inawadai fidia ya dola
milioni 490.9 za Kimarekani kwa kuiibia,
kuhujumu haki zake na kuisababishia hasara katika maslahi yake ndani ya IPTL.
Aidha imeomba Mahakama itoe tamko kuwa
benki hizo pamoja na mawakala wao hawajawahi kuwa wakopeshaji halali wa IPTL
pia wamefanya makosa ya wizi, kutakatisha fedha, na kusababisha hasara kwa
kampuni za IPTL na VIP kutokana na vitendo vyao.
No comments:
Post a Comment