WALIOPEWA URAIA RUKSA KUWANIA UBUNGE, UDIWANI


Wakimbizi 115,138 wanaoishi katika  makazi ya Mishamo na Katumba  mkoani Katavi, waliopewa uraia wa Tanzania, wana haki  zote  kama Watanzania wa kuzaliwa ya kuwapigia  kura madiwani , wabunge  na rais ,  katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Makazi ya Katumba wilayani Mlele, Athman Igwe  katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa (RCC).
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  mkoani humo, Laurent Magweshi, aliyetaka kujua iwapo wakimbizi waliopewa  uraia nchini, wana sifa ya kupiga kura  katika uchaguzi mkuu ujao  wa  Oktoba mwaka huu.
“Wakimbizi hao sasa ni Watanzania wapya na wana  haki  kama walizonazo Watanzania  wa kuzaliwa ya kupiga  kura  katika uchaguzi mkuu  ujao,“ alifafanua.
Aliongeza kuwa  wanayo haki pia ya  kujiandikisha  katika daftari la kudumu  la wapiga  kura  na  aliwahamasisha kujitokeza kwa wingi,  kujiandikisha ili waweze  kuipigia kura  Katiba inayopendekezwa Aprili 30 , mwaka huu .
“Watanzania hawa wapya  wanayo haki  ya kuchagua  na kuchaguliwa katika nafasi zote za uongozi  ikiwemo  nafasi  ya ubunge,  lakini  hawaruhusiwi  kugombea  nafasi ya urais,” alisisitiza
Alibainisha kuwa wakimbizi wapatao 115,138  wanaoishi kwenye Makazi  ya Mishamo na Katumba, wamepewa uraia wa Tanzania, katika mpango wa ugawaji vyeti unaoendelea, ambapo  62,544 wanatoka makazi ya Katumba wilayani Mlele  na  52,594 makazi ya Mishamo  wilayani Mpanda.
Akiwasilisha taarifa ya ugawaji wa vyeti vya  Watanzania wapya  waliokuwa wakiishi kwenye mkazi hayo, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Ignas Kikwala  alisema makazi ya Katumba yalipokea  wakimbizi 2,800  mwaka 1973 na mwaka 1978 Serikali ilianzisha  Kambi ya wakimbizi ya Mishamo  ikiwa na wakimbizi 12,000 .
Ugawaji vyeti kwa Watanzania hao   ulianza Novemba 26, mwaka jana na  utakamilika Aprili 30 mwaka huu  kwa makazi  ya Katumba na Mishamo  na Ulyankulu mkoani Tabora .

No comments: