WATANZANIA 99 WAFICHA BILIONI 200 USWISI


Kushamiri kwa fedha haramu nchini kunakofanywa na baadhi ya Watanzania wasio waaminifu ndani na nje ya nchi, kumeisababishia taifa hasara ya bilioni 590/- (dola milioni 328) kila mwaka, imeelezwa.

Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Rished Bade wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Akitoa ufafanuzi, Dk Bade alisema zipo taarifa mbalimbali zilizofanywa na mashirika ya nje zinazoonesha  kuna tatizo la fedha haramu nchini, jambo ambalo hatua zimechukuliwa na utafiti wa jambo hilo unaendelea kubaini ukweli wake, lakini hilo linawezekana kwani wapo watanzania wanaofanya biashara na kukwepa kulipa kodi.
“Ripoti ya Benki ya Kimataifa ya HBSC yenye makao yake Uingereza, ilitoa taarifa za akaunti zenye fedha haramu zinazofanywa na makundi mbalimbali, na Tanzania imetajwa kuwepo, sasa hawa watu wanatumia mbinu nyingi kuhakikisha wanaikosesha nchi mapato”, alisema Dk Bade.
Alisema  kiwango hicho cha dola milioni 328, ni kikubwa na kwamba matukio hayo yanafanywa na watanzania wasio waaminifu, ambao hutumia mbinu nyingi za biashara kudanganya kiwango halali cha fedha walichokipata kwenye biashara husika.
Awali akizungumza mbele ya kamati hiyo, Dk Bade alisema fedha haramu zinatokana na baadhi ya wafanyabiashara au watu wengine kufanya biashara nje ya nchi au kuingiza, lakini hawatoi takwimu sahihi, jambo ambalo wanakwepa kulipa kodi.
“Unakuta mtu amefanya biashara nje ya nchi, na hatoi takwimu sahihi, anaweza kuwa ameuza tani mfano laki mbili, ila anasema ameuza tani laki moja sasa hiyo tani laki moja nyingine  iliyouzwa haikatwi kodi, na ndiyo fedha haramu zenyewe hizo”, alisema Dk Bade.
Alifafanua kuwa kwa kutambua tatizo hilo, hivi sasa nchi imesaini Mkataba wa Kimataifa wa kupata taarifa za kodi kutoka mataifa mbalimbali duniani, ili kupata takwimu sahihi za watanzania wanaofanya biashara nje na kukwepa kodi.
“Jambo hili ni baya kwa ukuaji wa uchumi wetu, ila tumesaini Mkataba wa Kimataifa wa kupata taarifa za kodi, tumesaini mkataba huo Februari mwaka huu, utatusaidia kupata taarifa za watu wanaofanya biashara nje, na wasiolipa kodi halali,” alisema Dk Bade.
Wakati huo huo, Naibu Gavana wa Benki Kuu (BoT), Juma Reli alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kubanwa na kamati hiyo iliyomtaka kueleza Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 na Waraka uliotoka mwaka 1998, unaoelekeza ufunguaji wa akaunti nje ya nchi.
Katika maswali ya kamati hiyo, BoT ilihojiwa iwapo inatoa vibali vya watu kufungua akaunti nje ya nchi.
Akijibu hoja hiyo, gavana huyo alisema benki haitoi vibali kwa Watanzania waishio nchini, kufungua akaunti kwenye benki zilizo nje ya nchi, kwa kuwa sheria hairuhusu, ila kampuni za madini zinaruhusiwa, baada ya benki hiyo kuzipa vibali.
Kadhalika, pia watanzania waishio nje wanaweza kufungua akaunti kwa kuwa hawaishi nchini na pia kwa watumishi wa mashirika ya kimataifa waishio nje au kufanya kazi nje ya nchi.
Aliongeza kuwa hadi sasa hawana taarifa za watu binafsi wenye akaunti nje ya nchi, kwa kuwa kama wapo wamefanya hivyo bila vibali na ni kosa, lakini njia za kuwafuatilia ni ngumu kwa kuwa  hawana mfumo wa kupata taarifa kutoka benki hizo.
Jibu hilo lilisababisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto kuishauri serikali kuomba kupewa taarifa kutoka nchi za Uswisi na Uingereza za Watanzania wenye akaunti nje ya nchi.
Aidha, Zitto alihoji kwa gavana, iwapo benki ya HBSC, ina kibali cha kuja kuwafungulia akaunti wateja wa kitanzania na kama sio hatua gani zimechukuliwa.
Akijibu hoja hiyo, Gavana alisema, sheria hairuhusu benki hiyo kuja kufanya shughuli za kibenki nchini na kwamba kama benki hiyo imefanya hivyo, imevunja sheria  ila BoT haina taarifa.
“Hatuna taarifa kama HSBC wamekuja Tanzania kukutana na wateja wake, na kama wamekuja wamevunja sheria”, alisema Reli.
Pamoja na hayo, kamati ilitoa maagizo kwa vyombo hivyo viwili, yaani BoT na TRA kuhakikisha wanakuwa na utaratibu  baina yao wa kufuatilia walipa kodi ili wajulikane na kuondoa tatizo la ukwepaji kodi, unaosababisha uwepo wa fedha haramu nyingi.
Aidha BoT, imeagizwa kufuatilia benki hiyo ya HSBC, na kuichukulia hatua kwa kuvunja sheria za kufanya biashara na wateja wa hapa nchini kinyume na utaratibu, ili mabenki mengine yafahamu kuwa Tanzania sio nchi ya kuichezea.
Hata hivyo, Gavana Reli alisema mwishoni mwa mwaka huu kamati inayosimamia utafiti kuhusu fedha haramu nchini Tanzania, iliyoundwa mwaka 2012, ikiwashirikisha wadau kutoka nje ya nchi itapokea taarifa ya suala hilo, na itawekwa wazi kwa umma.
Hivi karibuni ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ), ulifichua kuwepo kwa Watanzania 99, wenye akaunti za siri nchini Uswisi zenye mabilioni ya fedha.
Taarifa ya Swiss Leaks ilionesha kuwa Watanzania hao, wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114, ambazo ni sawa na Sh bilioni 199.6.
Ripoti hiyo ilitokana na aliyekuwa mfanyakazi wa Benki ya Kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya yeye kuacha kazi.

No comments: