Tume ya Uchaguzi imesema
hata ikipokea barua kutoa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma
Kaskazini Zitto Kabwe haina uwezo wa kuchukua hatua yoyote mpaka watakapopokea
barua kutoka kwa Spika wa Bunge.
Akizungumza na mwandishi, Mkuu wa Idara ya Elimu ya Mpiga
Kura na Habari wa NEC, Ruth Masham,
alisema mpaka sasa hakuna barua iliyofika katika ofisi hiyo kutoka Chadema na
hata kama ikifika Tume ya Uchaguzi
haitatoa uamuzi wowote mpaka watakapokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge ambaye
kisheria yeye ndiye anayetoa taarifa kama kuna jimbo lipo wazi.
Alisema kama tukio hilo la kuvuliwa uanachama kwa Zitto ni lazima barua ya Spika ifike
ikitangaza kuna jimbo liko wazi ndio Tume ya Uchaguzi wanaweza kufanya maamuzi
na sio barua ya chama au mtu yeyote kutoka chama chochote.
Aliongeza kuwa
kisheria mwenye mamlaka ya kutaarifu Tume masuala ya nafasi iliyopo wazi ni Spika wa Bunge pekee na hawawezi kutumia habari zilizopo kwenye
vyombo vya habari na kuchukua maamuzi.
“Lazima tupate barua ya Spika ikitangaza kama kuna eneo
ambalo mbunge wake amevuliwa uanachama , amefariki, au ana matatizo ambayo
yanamfanya ashindwe kuendelea kuwa mbunge,” alisema Masham.
Wiki hii, Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitupilia mbali kesi ya madai iliyofunguliwa na
Zitto dhidi ya chama chake.
Jaji Richard Mziray alitupilia mbali kesi hiyo baada ya kukubali pingamizi la awali
lililowasilishwa na Chadema kupitia mawakili wake Peter Kibatala, Tundu Lissu
na John Mallya ambao walidai kesi hiyo ilifunguliwa bila kufuata utaratibu wa
sheria.
Aidha, Tundu Lissu ambaye ni Mkurugenzi wa Sheria wa
Chadema alisema: “Kwa mujibu wa katiba
ya Chadema, mwanachama yeyote anapofungua kesi mahakamani dhidi ya chama chake,
endapo atashindwa katika kesi hiyo atakuwa amejiondoa uanachama wake, kwa hiyo
natangaza rasmi Zitto Kabwe sio mwanachama tena wa Chadema.
Kuhusu utambulisho wa Zitto bungeni, Lissu alisema kwa
mujibu wa kanuni za chama chake, Katibu wa chama chake anatakiwa kumwandikia
barua Mwenyekiti au Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kumjulisha Zitto tena si
mwanachama wao na taratibu zingine zitafuata.
Naye, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, amebainisha
kuwa endapo Bunge litapata taarifa rasmi ya Chadema kumvua uanachama Zitto,
lazima Bunge hilo lifanye kwanza uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili ndipo
litoe uamuzi.
No comments:
Post a Comment