Msichana mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ni mjamzito au ana mtoto,
imeelezwa.
Idadi hii inawakilisha maisha halisi na kuonesha kwamba kama
jitihada za makusudi hazitachukuliwa wasichana wataendelea kukosa haki zao za
msingi na kuzidi kuwa wategemezi.
Hayo yalisema na mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akifungua mkutano wa
kimataifa wa utafiti katika ukunga ulioandaliwa na LUGINA
Afrika Midwives Research Network (LAMRN) uliofanyika katika Hoteli ya Kunduchi
jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) alisema vifo vya akinamama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni tatizo
katika nchi zote zilizopo Kusini mwa Bara la Afrika hata hivyo jitihada
mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua au kumalizika
kabisa.
“Naamini utafiti uliofanywa na LAMRN kwa kipindi cha miaka
miwili, utasaidia kuongeza utendaji kazi wa wakunga na kupunguza vifo vya
akinamama wajawazito na watoto katika bara letu la Afrika,” alisema.
Kuhusu mimba za utotoni Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema
tafiti zilizofanyika zinaonesha wasichana
wanaanza kufanya mapenzi mapema zaidi wakiwa na umri mdogo ukilinganisha
na wavulana jambo linalopelekea kupata mimba za utotoni na hivyo kukosa elimu
kwa kukatisha masomo yao.
Mama Kikwete alisema: “Takwimu za Ulimwengu zinaonesha zaidi
ya wasichana milioni 58 wameolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 kati ya hao milioni 15 wana umri wa miaka 10
hadi 14”.
Nchini Tanzania asilimia 13 ya wasichana wanaanza kufanya
mapenzi wakiwa na umri wa miaka 15 na kwa upande wa wavulana kwa umri huo huo ni asilimia saba".
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Seif Rashid, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema kaulimbiu ya mkutano huo ambayo ni 'utendaji
wa kazi kwa kutumia ushahidi wa utafiti, utaimarisha afya ya mama na watoto
wachanga' imekuja wakati muafaka wa kuweka suala la afya ya mama na mtoto kwanza
hii ni moja ya mipango ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa mwaka 2010-2015 katika bara la Afrika.
No comments:
Post a Comment