WALIOKUFA AJALI YA BASI MAFINGA SASA WAFIKIA 50


Miili ya watu wanane tu kati ya watu 50 walikufa katika ajali ya juzi, iliyohusisha basi na lori katika eneo la Changarawe, Mafinga mkoani Iringa, ndiyo iliyotambuliwa mpaka mchana.

Idadi ya marehemu wa ajali hiyo iliongezeka kutoka 42 waliokufa mapema juzi hadi 50. Mmoja wa hao walioongezeka aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa, ametambuliwa kuwa ni Oswald Mwinuka (58).
Wakati taarifa ya awali kutoka vyanzo mbalimbali ilidai wengi waliokufa katika ajali hiyo, walikuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi inaonesha wanaoendelea kutambuliwa walikuwa wafanyabiashara wa eneo la Soweto, mjini Mbeya.
Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania namba T 689 APJ mali ya Cipex Company lililokuwa likiendeshwa na Maka Sebastian (26) ambaye amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa akiendelea na matibabu na basi aina ya Scania namba T438 CED mali ya kampuni ya Majinja lililokuwa likiendeshwa na Baraka Gabriel (38) aliyekufa papo hapo juzi.
Wakati lori hilo lilikuwa likielekea barabara ya Mafinga-Mbeya, basi hilo lilikuwa likitoka Mbeya kuelekea jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa barabara katika eneo la ajali na mwendo kasi.
Baada ya magari hayo kugongana, kontena lililokuwa limepakiwa katika lori hilo lilifyatuka na kupiga basi hilo, hali iliyosababisha mauti na majeruhi wengi katika ajali hiyo.
Alisema zoezi la kutambua miili hiyo linaendelea katika hospitali ya mkoa wa Iringa na ile ya wilaya ya Mufindi mjini Mafinga.
Alisema imekuwa ngumu kutaja majina ya watu wote waliokufa kwa kuwa hawajatambuliwa na kuthibitishwa na ndugu zao.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Robert Salim alisema kati ya maiti 27 waliofikishwa hospitalini hapo juzi kutoka Mafinga ni wanane tu waliotambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao, wengi wao kutoka jijini Mbeya.
Kamanda Mungi alitaja miili iliyotambulikuwa kuwa ni Mbezi Deogratius  (29), Editha Ngunangwa (28), Mohamed Juma (32) na Ndenya Sixbert (25) ambao wote walikuwa wakazi wa Soweto Mbeya.
Wengine ni James Kinyamaguho (30) mkazi wa Morogoro, Said Halfan (35) na Abuu Mangula (35) ambao pia ni wakazi wa Mbeya.
Aliwataja waliojeruhiwa ambao wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa na ya wilaya ya Mufindi ya Mafinga kuwa ni Mustafa Ally, Dominic Shauri, Tito Kyando, Martin Haule, Ipyana Mbamba, Fadhil Kalenga, Mussa Mwasege, Nehemia Mbuji, Josam Abel, Tumpate Mwakapala, Nico Hamis na Ester William.
Wengine ni Peter Mwakanale, Kelvin Mwakaladi, Raphael Nerbot, Maga Sebastian, Catherine Mwijungu, Lucy Mtanga, Debora Vicent, Ester na mwanaume ambaye jina lake halijaweza kujulikana kutokana na kuwa na hali mbaya.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Salim alisema hali za majeruhi wanne waliolazwa hospitali ya rufaa ya Iringa inaendelea vizuri wakati wengine wanne hali zao sio nzuri na wanatarajia kupewa rufaa kwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Boaz Mnenegwa alisema hali za majeruhi 13 waliobaki Mafinga zinaendelea vizuri.
Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF) kimetoa salamu za pole na rambirambi kwa ndugu wa waliopoteza maisha na majeruhi wote wa ajali hiyo.
"Tukio hili ni baya sana na la kusikitisha kwa Watanzania. Si rahisi kuelezea tukio hili bila kulengwa ama kutokwa na machozi," ilisema taarifa hiyo.
Chama hicho kimeeleza kuwa matukio ya namna hiyo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na hakuna hatua za mashiko za kumaliza tatizo hili. "Kwa ajali hii licha ya uzembe waliofanya madereva, lakini miundombinu ya eneo la ajali haiko sawa kutokana na mashimo yaliyopo."
Kilieleza kuwa barabara nyingi za lami Tanzania zimeharibika sana na marekebisho yake huwa yanaweza yasifanyike ama yakafanyika kidogo kiubabaishaji.
"CUF tunaitaka serikali kupitia upya mfumo wake wa marekebisho ya barabara ili kuhakikisha ubovu wa barabara hauchangii kabisa katika kuleta ajali barabarani. Japo hii si tiba ya ajali za barabarini lakini kwa kiasi fulani itapunguza," alieleza taarifa hiyo.
Chama hicho kimeitaka Serikali iwawajibishe viongozi wake wazembe wanaotakiwa kupambana na ajali hizi, lakini hawatimizi majukumu yao.

No comments: