Wafanyabiashara watatu na wanachuo watano wamepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Singida wakikabiliwa na mashitaka ya kumdhalilisha kupindukia askari
polisi wa kike na kumsababishia maumivu
makali mwilini.
Mwanasheria wa Serikali, Petrida Mutta alidai mbele ya Hakimu Joyce Minde, kwamba kwa pamoja, washitakiwa hao walimfanyia unyama askari huyo kwa kumvua nguo zote na kumwacha mtupu kisha kumshambulia na kumsababishia maumivu makali mwilini.
Waliopandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Joyce
Minde, ni Jasmin Iddi (40), Abdallah
Hamduni (26), Ramadhani Bakari (32) wote wafanyabiashara wa mjini hapa pamoja
na dereva, Saidi Saidi (50) .
Wengine ni Aurelia
Adolf Mushi (20), Grace Daniel Paul (21), Happiness Kiluvya (23), Jackline John
(20) na Constansia Masaki (21) wanaodaiwa ni wanachuo katika moja ya vyuo vya
elimu ya juu mjini Singida.
Mwanasheria wa serikali, alidai wakati wote wa kitendo hicho cha
udhalilishaji, polisi huyo, alikuwa akichukuliwa picha za video huku akiwa
mtupu na kuzisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Tukio hilo inadaiwa lilifanyika Februari 14, mwaka huu
saa 11.30 jioni ambako kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka, inadaiwa polisi huyo
wa kike alikutwa akiwa na mume wa mshitakiwa,
Jasmin wakiwa kando ya Ziwa Singidani wakivinjari siku hiyo ya
Wapendanao.
Hata hivyo, mume
ambaye jina halikupatikana, inadaiwa
alitoroka. Mutta alidai mbele ya mahakama hiyo kuwa kitendo walichofanya
washitakiwa ni kinyume na Kanuni ya Adhabu 138 A kifungu cha 16 cha Mwenendo wa
Makosa ya Jinai kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wote walikana mashitaka.
No comments:
Post a Comment