SHERIA YATUNGWA KUDHIBITI OMBAOMBA

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam inakusudia kutunga sheria kadhaa ndogo, ikiwemo ya kudhibiti ombaomba na uendeshaji wa soko la samaki Feri.

Sheria nyingine zinazotarajiwa kutungwa ni pamoja na sheria za zao la ngozi na za mfuko wa elimu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Halmashauri ya Ilala ambayo imesainiwa na Mkurugenzi wake, Isaya Mngurumi imesema mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa kifungu cha 89 cha sheria za Serikali za Mitaa Mamlaka za Miji sura ya 288 ya mwaka 2002.
Aidha, sambamba na mabadiliko hayo, vilevile halmashauri hiyo inakusudia pia kufanya marekebisho katika sheria nyingine ndogo  ambazo ni sheria ya usafi wa mazingira, kodi za majengo na matumizi ya barabara.
Halmashauri hiyo imewataka wananchi pamoja na wadau wote kujitokeza kutoa maoni yao na mapendekezo kuhusu utungaji wa marekebisho ya sheria hizo zilizotajwa.
Aidha, maoni hayo yametakiwa kuwasilishwa kwa njia ya maandishi katika ofisi za watendaji kata, ofisi ya mkurugenzi idara ya sheria katika ofisi za Arnautouglo Mnazi Mmoja kabla ya Machi 31, mwaka huu.

No comments: