‘WAGANGA’ WALAANI MAUAJI YA ALBINO


Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili Tanzania limelaani  mauaji wanayofanyiwa walemavu wa ngozi, vikongwe na kunajisi watoto yanayofanyika kwa baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa chama hicho, Abdulrahman Lutenga alisema wameumizwa na mauaji hayo wanayotendewa walemavu wa ngozi ambayo yametokea katika mikoa 10,  Mwanza matukio 13, Kagera matukio sita, Tabora matukio matano, Geita matukio manne na Mara matukio manne.
Alisema  sababu za mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, vikongwe na kunajisi watoto ni matapeli wanaojifanya waganga wa tiba asili wakiwadanyanya watu wanaweza kuwatajirisha watu kama wakileta viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Waganga  hao matapeli wanatoa masharti kwa wateja wao na wakishindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa mganga huyo tapeli anampa mteja masharti magumu ambayo hayatekelezeki kiurahisi na kwa uwazi kama kuleta viungo vya albino, kuua na kubaka vikongwe na kubaka watoto wadogo.
Aliongeza kuwa mauaji hayo yanachangiwa pia na watu kuwa na uroho wa madaraka makubwa na kuwa na imani potofu kuwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinaweza kuwa na mvuto wa mali.
Pia alisema sababu nyingine inayosababisha mauaji haya ni pamoja na ukosefu wa elimu watu hawana hofu ya mungu  tamaa ya mali na serikali kuchelewa katika upelelezi na kutoa hukumu kali kwa wanaobainika na viungo vya wenye ulemavu wa ngozi.
Alisema ili kudhibiti mauaji haya ni vyema elimu ikatolewa kwa jamii nzima ili kuondoa imani potofu kuhusu albino macho mekundu kwa vikongwe ubakaji na kunajisi watoto.
Pia alisema serikali ifanye upelelezi kwa haraka na wawabane na kupewa adhabu kazi wale wote watakaopatikana na viungo au kujihusisha na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ili waweze kutaja mtandao mzima wa wahusika.
Alitoa mwito kwa wananchi kuwa makini na wasikubali kutapeliwa kwa kupitia waganga matapeli na ramli chonganishi kwani hakuna mafanikio yanayopatikana kwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi na hakuna mganga anayeweza kumpatia mtu utajiri njia pekee ya kutajirika ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii.

No comments: