MFUMUKO WA BEI WAONGEZEKA


Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumko wa bei wa taifa kwa mwezi Februari umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.2 kutoka asilimia 4.0.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa NBS, Ephrahim Kwesigabo alisema hiyo inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Februari 2015 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo  kwa mwaka ulioishia Januari mwaka huu.
Alisemaa fahirisi za bei zimeongezeka hadi 154.83 kwa mwezi Februari kutoka 148.62 mwezi Februari mwaka jana. Aliongeza kuwa mfumko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Februari 2014 umeongezeka kwa kasi ya asilimia 4.9 kama ilivyokuwa Januari mwaka huu.
Kwesigabo alisema kuongezeka kwa mfumko wa bei wa mwezi Februari  kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Februari 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari  2014.
Alitoa mfano wa mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kuongezeka mwezi Februari 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari mwaka jana ni pamoja na bei za mchele, unga wa mhogo, nyama, samaki na maharage.
Aliongeza kuwa mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula ambazo bei yake iliongezeka mwezi Februari mwaka huu ni mavazi ya wanaume, mavazi ya wanawake, mkaa, mashuka na gharama za kumwona daktari ambazo nazo ziliongezeka kwa asilimia 11.2.
Kuhusu mfumko wa bei wa mwezi Februari unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 1.6, ukilinganisha na ongezeko la asilimia 1.0 mwezi Januari 2015.
Alisema fahirisi za bei zimeongezeka hadi 154.83 mwezi uliopita kutoka 152.43 ya Januari. Kwesigabo alisema kuongezeka kwa fahirisi  kulichangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Alisema mfumko wa bei nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki na akatoa mfano  kuwa mwezi uliopita mfumko wa bei uliongezeka kwa nchi zote tatu za Kenya, Uganda na Tanzania. Uganda mfumko uliongezeka hadi asilimia 1.4 kutoka 1.3, Kenya ulifikia asilimia 5.61 kutoka 5.53.

No comments: