TRENI IENDAYO KASI KWENDA BARA KUANZA APRILI


Shirika la Reli Tanzania (TRL) limetangaza nauli ya treni mpya ya Deluxe,  zilizoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), zitakazoanza kutumika mapema Aprili, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TRL iliyotolewa jana, nauli hizo ni kutoka vituo vya Dar es Salaam kwenda Kigoma, Kigoma kwenda Dar es Salaam na Mkoa wa Mwanza.
Nauli hizo ni kati ya Sh 77,800 kwa daraja la kwanza ambalo ni la kulala.
Kwa kituo cha Dar es Salaam kwenda Kigoma, nauli zilizoidhinishwa ni kwenda Morogoro daraja la kawaida nauli itakuwa Sh 10,900, daraja la pili nauli itakuwa Sh 14,600 na daraja la kwanza nauli itakuwa Sh 24,300.
Nauli kwenda Dodoma itakuwa  Sh 18,500 kwa daraja la kawaida, Sh 24,700 kwa daraja la pili na Sh 41,200 kwa daraja la kwanza, huko nauli kwenda Tabora kutoka Dar nauli ni Sh 25,400 kwa daraja la kawaida, Sh 33,900 daraja la pili na Sh 56,500 kwa daraja la kwanza.
Nauli kwenda Kigoma daraja la kawaida ni Sh 35,700 daraja la pili ni Sh 47,600 na daraja la kwanza ni Sh 79,400 na kwa kituo cha Kigoma  kwenda Dodoma nauli ni Sh 23,600 daraja la kawaida, daraja la pili ni Sh 31,400 na daraja la kwanza ni Sh 52,400.
Aidha, nauli kutoka Kigoma kwenda Morogoro ni kati ya Sh  30,900 hadi Sh 68,600 kulingana na daraja na kwamba kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam nauli ni kati ya Sh 6,200 hadi 77,800 kulingana na umbali na daraja.
Mfano, kutoka Mwanza kwenda Malampaka nauli daraja la kawaida ni Sh 6,200 daraja la pili ni Sh 8,300 na daraja la kwanza ni Sh 13,800 na nauli kutoka Mwana kwenda Dodoma nauli ni kati ya Sh 22,800 hadi Sh 50,600 kulingana na daraja.
Na nauli kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam nauli Sh 35,00 kwa daraja la kawaida, daraja la pili Sh 46,700 na daraja la kwanza Sh 77,800.
Awali akizungumzia usafiri huo, Meneja Biashara wa Kampuni ya Deluxe, Charles Ndenge alisema  usafiri wa treni hizo ni wa kasi na utatumia saa 30, kufika  katika mikoa mbalimbali ambayo reli ya TRL inapita  na kusimama kwenye vituo vikubwa 14, kati ya vituo 54, vilivyopo.
Alisema treni hiyo ya Deluxe itafanya safari zake mara moja kwa wiki kwa kupokezana na mikoa ya Kigoma na Mwanza na kuwa itatumia mabehewa yenye ubora na kupunguza msongamano.
“Kutakuwa na behewa moja zuri la huduma za chakula na vinywaji na mawasiliano”, alisema Ndenge.
Akizungumzia muundo wa treni hiyo ya Deluxe, alisema itakuwa na mabehewa 10 ya daraja la tatu, ambapo kila moja litabeba abiria 80, mabehewa manne ya daraja la pili kila moja litabeba abiria 60, wa kukaa na mabehewa sita ya kulala ya daraja la kwanza kila moja litabeba abiria 36.
Aidha aliongeza vichwa vya treni  vimejengwa upya na kuwekewa teknolojia mpya na kutengenezwa makochi mapya.

No comments: