`ALIYEFICHA’ WATOTO 18 MOSHI AJITETEA


Siku mbili baada ya jeshi la polisi kuvamia nyumba moja katika Kata ya Pasua  katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, iliyotumika kuhifadhi zaidi ya watoto 18 kinyume cha utaratibu, mmiliki wa nyumba hiyo yenye vyumba vinne na choo kimoja, ameibuka na kujitetea licha ya kwamba anashikiliwa na polisi.

Mmiliki huyo, Abdulnasir Abdulrahman amesema aliwakusanya watoto hao wenye umri wa kati ya miaka miwili na 16 ili kuwafundisha masomo ya dini ya Kiislamu na kuwakuza katika imani hiyo wakiwa wadogo.
Pamoja na utetezi huo, alisema  watoto hao wameletwa hapo na wazazi wao kupata elimu ya dini, na wazazi wao wanajua na wanachangia vitu mbalimbali, ikiwemo vyakula ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya dini ya kiislamu,
“Watoto wote tunaoishi nao hapa wana wazazi wao, ambapo wamekubaliana na sisi waaendelee kupata elimu hiyo hapa chini ya uangalizi wetu na wazazi wao wamekubaliana niwalee,” alisema Abdulrahman jana baada ya kukamatwa majira ya saa 5 asubuhi, tukio lililovutia umati wa wakazi wa mji wa Moshi waliofurika katika nyumba hiyo na hata Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Moshi.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Geofrey Kamwela alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na pia baadhi ya wazazi wa watoto hao kwa uchunguzi zaidi.
Katika nyumba waliyohifadhiwa watoto hao, polisi wenye silaha walilazimika kutumia nguvu na mabomu kudhibiti umati wa wananchi waliojitokeza kushuhudia kukamatwa kwa mmiliki na watoto.
Baada ya kufikishwa polisi, walirudishwa katika nyumba waliyokuwa wamehifadhiwa wakiwa chini ya ulinzi, huku mmiliki na wazazi wakiendelea kubaki polisi.
Jeshi la polisi linawashikilia baadhi ya wazazi na mmiliki wa nyumba hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi, ambapo baada ya watuhumiwa hao kukamatwa bado mamia ya wananchi hao waliongozana hadi kituo cha polisi. Hadi gazeti hili linaenda mitamboni, bado wananchi walikuwa wamefurika nje ya geti hilo la kituo cha polisi.
Akizungumza na wananchi katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga alisema walipata taarifa kuwa eneo la Pasua, kuna mtu mwenye kituo amehifadhi watoto kinyume na taratibu, na ndiyo kamati ya ulinzi na usalama ilifika eneo la tukio na kukuta watoto  hao katika nyumba hiyo.
Alisema taarifa ya kuwepo kwa watoto hao waliipata wiki moja iliyopita, lakini juzi Machi 7,  mwaka huu,  ndiyo jeshi la polisi liliizingira nyumba hiyo kuanzia majira ya saa 12:05 jioni  kutokana na kukosa sehemu ya kuwahifadhi watoto hao
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwakusanya watoto sehemu moja bila kibali ni kinyume cha sheria, ambapo mmiliki wa nyumba hiyo alipaswa kuomba kibali lakini pia mafunzo anayoyatoa kwa watoto hao hata kama ni masuala ya dini ni lazima yafuate taratibu za nchi.
“Sheria zipo unapokusanya watoto mahala pamoja kunatakiwa kuweje kuanzia mazingira hadi eneo lenyewe, na kama una taasisi unaendesha mafunzo, je, kituo kimesajiliwa na ndiyo maana tumeagiza watoto warudishwe kwa wazazi wao,” alisema Makunga.

No comments: