Upande wa
utetezi katika kesi ya jinai inayomkabili kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda
umewasilisha hoja zitakazoifanya mahakama kutoona sababu kwa mshitakiwa huyo
kuwa na kesi ya kujitetea.
Mawasilisho
hayo yalifanywa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro,
Mary Moyo kwa zaidi ya saa tatu na mawakili Juma Nassoro na Abubakar Salim,
wanaomtetea Ponda.
Akitoa
mawasilisho hayo, Wakili Nasoro alidai kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa
mashtaka pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo, unatia shaka na una
udhaifu mkubwa, unaomfanya mshitakiwa akose kesi ya kujibu.
Alidai
pia hati ya mashtaka yenye makosa matatu, inaonekana kuwa na mapungufu hasa
katika shtaka la kwanza, kwani imeshindwa kueleza ni kwa namna gani mshtakiwa
huyo alikiuka amri ya mahakama, kama alivyoshitakiwa katika hati hiyo.
Alidai
kuwa licha ya kushtakiwa kwa kosa la kutotii amri halali ya mahakama,
iliyotokana na hukumu, upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha hukumu hiyo
kama sehemu ya ushahidi.
Wakili
huyo alidai kuwa hukumu iliyotolewa Mahakama ya Kisutu dhidi ya Ponda, haina
amri yoyote inayoonesha kuwa imetengeneza kosa kwa Shehe Ponda, bali inaweza
kuwa ni kukiuka masharti, ambayo sio kosa la jinai.
Baada ya mawasilisho hayo, upande wa mashtaka
uliiomba muda mahakama kujibu hoja zilizokuwemo kwenye mawasilisho hayo.
Mahakama iliridhia ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 20, mwaka huu
na hivyo mshtakiwa kurudishwa rumande chini ya ulinzi mkali wa polisi.
No comments:
Post a Comment