Hali
ya ukame inatarajiwa kukabili nchi kutokana na upungufu wa mvua utakaoathiri
pia upatikanaji wa nishati ya umeme.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
imehadharisha juu ya hali hiyo na kutaka mamlaka zinazohusika na masuala ya
umeme, kuanza kuchukua njia mbadala wa uzalishaji nishati kutokana na tishio
hilo.
Aidha, upungufu wa unyevu ardhini kutokana na
vipindi vya ukosefu wa mvua, umetajwa kuwa utaathiri shughuli za kilimo katika
maeneo mengi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Agnes Kijazi
(pichani) alitoa taarifa hiyo wakati wa kutoa mwelekeo wa mvua za masika kwa
kipindi cha Machi, Aprili na Mei mwaka huu.
Alisema kwa kipindi hicho, mvua haitarajiwi kuwa
ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi.
Alisema mvua za wastani na juu ya wastani, zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo
hususan Kanda ya Ziwa Victoria na maeneo
ya kusini mwa nchi.
Mvua zitaanza mapema katika maeneo ya Kanda ya
Ziwa Victoria na baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini.
“Pamoja
na kuwapo kwa uwezekano wa matukio ya mvua kubwa katika maeneo yanayotarajia
kupata mvua juu ya wastani, hali hiyo pia inaweza kujitokeza katika maeneo
yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani,” alisema Kijazi.
Maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, mvua
zinatarajia kuanza mapema na pia kuwapo kwa vipindi vifupi vya ukame katika
maeneo mengi hususani Machi na Mei.
Mvua zilianza wiki ya nne ya Februari katika mikoa ya Kagera, Geita, Mara
na Mwanza, huku kanda hiyo ya Ziwa ikitarajia kupata mvua za wastani na juu ya
wastani. Kwa upande wa Mikoa ya Simiyu na Shinyanga, inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani.
No comments:
Post a Comment