Watu
wanne akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihanda na wazee wawili wa kimila wa kijiji
hicho wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusu kuuawa kwa wazee wawili mtu na mkewe.
Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Dodoma, David Misime wakati akitoa taarifa ya vifo vya watu watatu
vilivyotokea wilayani Kongwa, mkoani hapa Jumapili iliyopita.
Alisema watu waliokamatwa wanatuhumiwa kuhusika
na mauaji ya mume na mke, Peter Kaluli (85) na Kaila Kaluli (80) wakiwa
wamelala ndani ya nyumba yao ya tembe.
Aidha alisema kwamba watu hao waliuawa kwa
kuangushiwa ukuta wa nyumba yao kisha kuchomwa moto. Pia wanatuhumiwa kuhusika
na kubomoa nyumba nyingine mbili za tembe za kaya hiyo.
Alisema tukio hilo lilitokea kwenye kitongoji
cha Majengo, kijiji cha Ihanda, Kata na Tarafa ya Mlali wilayani Kongwa.
Kwenye tukio hilo watu hao walifanya uharibifu
mwingine kwa kuwaua nguruwe mmoja na kumkata miguu ng’ombe.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo
cha mauaji na uharibifu huo ni imani za kishirikina wakiwatuhumu vikongwe hao
kuwa wanazuia mvua kunyesha.
No comments:
Post a Comment