SUMATRA YAANZA MCHAKATO KUREKEBISHA NAULI ZA MABASI


Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imeanza mchakato wa mapitio ya viwango vya nauli za mabasi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, mapitio hayo yana lengo la kubaini haja ya kurekebisha viwango vya nauli za mabasi hapa nchini.
“ Kwa mujibu wa Sheria ya Sumatra ya 2001 na Kanuni zake, Mamlaka imeamua kufanya mapitio ya viwango vya juu vya nauli nchini kwa lengo la kubaini haja ya kufanya marekebisho. Ili kutumiza hili mamlaka inatakiwa kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kuridhia viwango vya tozo kwa huduma zinazodhibitishwa na mamlaka zikiwemo nauli za mabasi.”
SUMATRA imeandaa mikutano ya kupokea maoni ya wadau wa usafiri ikiwa ni pamoja na watoa huduma, watumiaji wa huduma na wananchi kwa ujumla.
Taarifa hiyo inaonesha ratiba ya mikutano ambapo mkutano wa kwanza umepanga kufanyika Jumatatu ijayo katika Ukumbi wa Gold Crest Hotel, utafuatiwa na mkutano wa Machi 12 utakaofanyika ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma na wa tatu utafanyika jijini Dar es Salaam Machi 18 katika ukumbi wa Karimjee.
Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Kutetea Abiria (CHAKUA), Godwini Ntongeji alisema awali waliiandikia SUMATRA kutaka washushe bei ya nauli ili wananchi waweze kunufaika na kushuka kwa bei ya mafuta iliyoanza kushuka kuanzia Januari mwaka huu.
“Awali tuliwaandikia barua SUMATRA, hawakutujibu, baada ya muda tukawaandikia barua ya kuwakumbusha na ndipo walipotujibu na tunashukuru tumeshaona matangazo ya kuwaita wadau katika kujadili nauli,” alisema.

No comments: