KOREA KUSINI KUTOA FEDHA ZA DARAJA JIPYA SELANDER


Serikali ya Jamhuri ya Korea ya Kusini hatimaye imekubali kutoa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja jipya la kisasa la Selander.

Korea imekubali kutoa mkopo wa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo jipya na la kisasa, ambalo litakuwa mbadala wa daraja la zamani la Selander.   
Daraja hilo litapita pembezoni mwa daraja la zamani la Selander kuanzia Coco Beach (Oysterbay)  hadi  Hospitali ya Aga Khan katika Barabara ya Barack Obama.
Kauli hiyo ilitolewa na Balozi wa Jamhuri ya Korea Kusini nchini, Chung Il wakati alipomwalika Waziri wa Ujenzi,  Dk John Magufuli na ujumbe wake katika chakula cha jioni nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam,  juzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Chung Il alisema kuwa fedha hizo za mkopo wa masharti nafuu, zitatolewa  kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Tanzania.
“Naomba tuendelee kudumisha uhusiano wetu hapa Tanzania pamoja na Korea Kusini na ndio maana kuna wananchi zaidi ya 500 kutoka Korea Kusini wanaoishi hapa Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake,  Dk Magufuli  alisema anaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea
Kusini kwa kuridhia kutoa fedha hizo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo la kihistoria nchini.
“Naishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kwa msaada mkubwa katika ujenzi wa daraja hili jipya na serikali hiyo ndiyo iliyowezesha pia ujenzi wa Daraja la Kikwete katika mto Malagarasi pamoja na ujenzi wa barabara ya kilomita 48 mkoani Kigoma,” alisema.
Alisema, “Daraja la Kikwete mkoani Kigoma limekwisha kamilika pamoja na barabara ya kilomita 48 kwa ubora mkubwa,  hivyo naamini kuwa hata ujenzi wa daraja hili jipya la Selander litakalopita baharini  litakuwa mfano wa kuigwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki”.
Daraja hilo jipya pamoja na barabara, litakuwa na urefu wa kilomita 7.2 na uwezo wa kupitisha magari zaidi ya 61,000 kwa siku. Ujenzi wa daraja hilo utaanza mwaka huu na wiki ijayo watatia saini mkataba wa ujenzi huo.
Korea Kusini itatoa asilimia 80 za ujenzi wa daraja hilo jipya, ambazo ni Sh bilioni 110  na asilimia 20 itatolewa na Serikali ya Tanzania. Daraja la kwanza katika eneo hilo la Selander,  lilijengwa na wakoloni mwaka 1929.

No comments: