Serikali imeahidi kumpatia kila Mtanzania
kitambulisho cha uraia mwaka huu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Pereira Ame Silima alisema hayo mjini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua
kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete
itaendelea kusaidia NIDA ili kufikia malengo ya serikali ya Awamu ya Nne ya
kila Mtanzania kuwa amesajiliwa na kupata kitambulisho chake.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maimu, alisema mpaka sasa NIDA
imepiga hatua kubwa katika suala la Usajili na Utambuzi wa watu na ugawaji wa
vitambulisho vya taifa.
Mpaka sasa NIDA imefanikiwa kusajili wananchi
milioni 6.1, ambapo kati ya hao, wananchi milioni 2.8 tayari wameshakamilisha
hatua za usajili kwa maana ya kuchukuliwa alama za kibayolojia kwa Zanzibar na
Bara. Jumla ya vitambulisho milioni 1.7 vimezalishwa na kugawanywa kwa
wananchi.
NIDA tayari imekamilisha usajili wa awali
Tanzania Zanzibar, mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro na
Tanga.
Akielezea changamoto kubwa ya sasa
inayoikabili Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Maimu alieleza changamoto kubwa
kuwa ni rasilimali fedha na rasilimali watu na hivyo kuzorotesha utendaji
na mikakati ya kuendelea na Usajili katika mikoa ya Tanzania.
"Mipango wa sasa ni kuanza rasmi kwa
matumizi ya vitambulisho vya taifa, na tayari vikao na wadau wanufaika vimeshafanyika
kwa Bara na Visiwani na muda si mrefu Vitambulisho vitaanza kutumika kama
nyaraka rasmi ya utambulisho," alisema.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Naibu Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira ameahidi serikali kupitia Wizara yake
kuendelea kuongezea nguvu Mamlaka kufikia malengo iliyojiwekea.
No comments:
Post a Comment