SERIKALI YAFUNGULIWA KESI 1,179 KWA MIAKA MINNE


Serikali imefunguliwa kesi 1,179 na wananchi , mashirika na taasisi mbalimbali, Bunge  lilielezwa. 
Kesi hizo ni kati ya kesi 1,192 zilizofunguliwa mahakamani kuanzia mwaka 2010 hadi 2014. Kati ya kesi hiyo Serikali imefungua jumla ya kesi 13 kama mshitaki. 

Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Ummy Mwalimu aliliambia Bunge kuwa katika kipindi cha 2010 hadi 2014 jumla ya kesi zilizosikilizwa na kumalizika mahakamani ni 591. 
Alisema kati ya kesi hizo zilizosikilizwa, Serikali imeshinda kesi 511 na imeshindwa kesi 80. Kesi ambazo bado zinaendelea kusikilizwa mahakamani ni 601. 
Ummy alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Amina Abdulla Amour  (Cuf) ambaye alitaka kufahamu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni kesi ngapi za kushitaki na ngapi za kushtakiwa kwa Serikali zimefunguliwa. 
Mbunge huyo pia alitaka kufahamu ni kesi ngapi Serikali imeshinda na zile ambazo imeshindwa. Katika swali lake la nyongeza mbunge huyo alihoji kwa nini Serikali imeshtakiwa mara nyingi na wananchi wake. 
Katika majibu yake ya nyongeza, Naibu Waziri alisema suala la wananchi kuishitaki Serikali ni suala la kikatiba na Serikali haina mamlaka ya kuzuia mtu asiishitaki mahakamani. 
Alisema inachofanya Serikali kwa sasa ni kuwaelimisha watendaji wake waamue na kutenda mambo kwa kufuata sheria za nchi; kwani kesi nyingi  dhidi ya Serikali kushitakiwa zinatokana na watendaji kufanya maamuzi bila kufuata sheria. 
Aliongeza kuwa licha ya hatua hiyo, Serikali pia iko kwenye juhudi kuhakikisha inaimarisha vitengo vya sheria katika taasisi, wakala na idara zake ili waweze kuwaelimisha watendaji kuhusu masuala ya kisheria.
Pia Mwalimu alisema Serikali inajitahidi kuwaelimisha wananchi wajue mipaka yao na wajibu wao kwa Serikali ili kuepusha mivutano baina ya taasisi za serikali na wananchi.

No comments: