HUKUMU YA MBUNGE WA BAHI APRILI 29


Hukumu ya kesi ya kuomba na kupokea rushwa inayomkabili Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel inatarajia kutolewa  Aprili 29, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hakimu Mkazi, Hellen Riwa anatarajia kutoa hukumu hiyo baada ya Mahakama kusikiliza na kupitia ushahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na pande zote mbili katika kesi hiyo.
Badwel anadaiwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka 2012, katika maeneo tofauti Dar es Salaam, alishawishi apewe rushwa ya Sh milioni nane kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana.
Inadaiwa Badwel aliomba rushwa hiyo ili awashawishi wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kupitisha hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
 Aidha anadaiwa Juni 2, 2012 katika Hoteli ya Peacock, iliyopo Ilala, alipokea rushwa ya Sh milioni moja kutoka kwa Sipora.
Katika utetezi wake, alidai hajawahi kuomba wala kupokea rushwa kutoka kwa Sipora na kuiomba Mahakama itende haki kwa kuwa tuhuma dhidi yake, zilikuwa ni njama za kumchafua.
 Alidai  Sipora katika ushahidi wake mahakamani, alikiri kuwa “sijawahi kumuomba rushwa pia kamati ninayodaiwa kutaka kuishawishi ina wajumbe 15 nisingeweza kuwashawishi kwa kuwa sina mamlaka hayo”.

No comments: