Watu
saba ambao wote ni wanaume wamekufa papo hapo na wengine 17 kujeruhiwa baada ya
basi walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda mjini Ifakara, wilayani
Kilombero mkoani Morogoro kupinduka ndani ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi
katika barabara kuu ya Morogoro –
Iringa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard
Paulo, alithibitisha jana kutokea kwa ajali hiyo majira ya saa sita mchana
maeneo ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi, wilayani Kilosa kwenye barabara kuu ya
Morogoro- Iringa wakati basi hilo
likitaka kulipita lori lililokuwa mbele yake na kukosa mwelekeo.
Kwa mujibu wa Kamanda Paulo, basi hilo lenye
namba za usajili T 637 CDC aina ya Tata, mali ya Kampuni ya Msanga Line Express
lililokuwa likiendeshwa na Saleh Rajabu (42), likitokea Dar es Salaam kwenda
Ifakara, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
Akielezea chanzo cha ajali hiyo, alisema wakati
mvua inanyesha gari hilo lililazimisha kulipita lori lililokuwa mbele yake
lililokuwa likielekea Iringa, ndipo gari hilo likakosa mwelekeo, kupinduka na
kusababisha vifo vya watu saba na kujeruhi wengine 17 waliokimbizwa Hospitali
ya Mtakatifu Kizito, Mikumi huku miili ikihifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Morogoro.
Hii itakuwa ni ajali ya pili kutokea ndani ya
hifadhi ya Taifa ya Mikumi, ambapo Machi 17, mwaka huu, watu wawili walifariki
dunia papo hapo na wengine 18 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali ya barabarani
baina ya basi la FM Safari na Mitsubishi Fuso katika barabara kuu ya Morogoro –
Iringa.
No comments:
Post a Comment