Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Viana Mulokozi ameibuka
mshindi wa Sh milioni 10 za shindano la 3N,
linaloendeshwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi.
Licha ya Viana ambaye ni mshindi kwa mwezi Februari,
washiriki wengine tisa ambao waliingia 10 bora walikabidhiwa Sh milioni moja
kila mmoja. Baadhi ya vijana hao ni
Irene Mateshi, Gelard Malamba, Edson Kashaija, Mjamaica Rabsa, Michael
Emanuel na Frank Mwasekagu.
Shindano hilo ambalo
linajulikana kama Nitabuni, Nitafanya na Nitafanikiwa (3N), limebuniwa na Dk
Mengi kwa ajili ya kuwapa fursa vijana kubuni miradi ya kibiashara ambayo
wanaweza kuiendesha.
Shindano hilo litaendeshwa kwa miezi sita na linaendeshwa
kupitia Tweet na Mengi na kila mwezi Dk Mengi anatoa Sh milioni 19 kwa ajili ya
washindi. Mwezi uliopita jumla ya tweeter zilizotumwa zilikuwa 5,069.
Viana katika wazo lake amesema ameanzisha mtandao maalum
ambalo utatumiwa na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kwa ajili ya kutafuta
mashirika na kampuni ambazo wanaweza kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo.
Alisema wanafunzi wengi walioko vyuo vya elimu ya juu kila
mwaka wanatakiwa kwenda kwenye mafunzo, lakini wengi wamekuwa wanaenda kwenye
kampuni kubwa wakati kuna kampuni ndogo ambazo zinawahitaji lakini
hawazifahamu.
"Nimekuja na
wazo hili kwa kutambua kuwa kuna kampuni zinahitaji wanafunzi lakini
hazifahamiki, hivyo ninaamini kuwa kwa kutumia mtandao huu, wanachuo wote
wataweza kupata mafunzo kwa vitendo kwa kulipia fedha kidogo badala ya
kuzunguka mjini kusaka nafasi kwenye kampuni mbalimbali," alisema.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Dk Mengi
aliwataka vijana kuacha tamaa ya kutaka utajiri wa haraka kitendo ambacho
kitawafanya waingie kwenye vitendo vya rushwa. Alisema utajiri wa namna hiyo
una laana ya Mungu.
Alisema ameanzisha shindano hilo kwa ajili ya kuwafanya
vijana waingie kwenye biashara ili waweze kuondoa ombwe la kiuchumi lilipo kati
ya nchi hii ambayo ni tajiri lakini watu wake ni masikini. Aliwataka vijana hao
wakifanikiwa wasisahau kuwasaidia wenzao ambao pia watakuwa ni wahitaji.
Pia,
aliwataka vijana hao kuepuka kuingia kwenye masuala ya kusema uongo ili
wafanikiwe na akaonya kuwa ni kufanya shughuli halali na kusema ukweli
kutawafanya wafanikiwe katika maisha yao.
No comments:
Post a Comment