HIKI NDIO CHANZO CHA MBU ANAYELETA HOMA YA DENGUE


Asilimia kubwa ya mazalio ya mbu Aedes aliyeambukiza virusi vya Dengue katika jiji la Dar es Salaam mwaka jana, huzaliwa kwenye vyombo vya plastiki na matairi ya magari, utafiti umebaini.

Aidha, kiwango kikubwa cha uwiano kati ya vyombo vinavyoruhusu maji kutuama na idadi ya nyumba, kinaashiria kuwepo kwa hatari ya mlipuko wa Dengue katika wilaya zote za Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela alisema katika nyumba 796 zilizofanyiwa ukaguzi katika wilaya tatu, asilimia 38.3 (nyumba 304) zilikuwa na vyombo vyenye maji yanayoruhusu kuzaliwa kwa mbu katika mazingira yake, huku asilimia 27.5 (nyumba 219) zilikutwa na vyombo vyenye viluwiluwi au mabuu ya mbu aina ya Aedes.
“Asilimia kubwa ya mazalio ya mbu yalikuwa ni vyombo vya plastiki vyenye ukubwa wa wastani vilivyoachwa wazi na kutohifadhiwa vyema na matairi ya magari.
Aliongeza: “Uwiano wa idadi ya vyombo vyenye mazalio ya Aedes kwa idadi ya nyumba zote zilikaguliwa ilikuwa ni asilimia 18.1 kwa Ilala, asilimia 35.3 kwa Kinondoni na asilimia 25.5 kwa Temeke.
Alisema uwiano wa vyombo vyenye viluwiluwi  kwa vyombo vyote vilivyokaguliwa ilikuwa ni asilimia 77.4 kwa wilaya ya Ilala, 65.2 Kinondoni na asilimia 80.3 Temeke huku asilimia 25.6 ya uchunguzi wa vinasaba katika mbu walikuwa na virusi vya dengue.
Akizungumzia maambukizi kwa binadamu, Malecela alisema kati ya wagonjwa 483 waliofanyiwa utafiti  asilimia 20.9 walikuwa wajonjwa wenye maambukizi mapya na asilimia 1.9 maambukizi ya zamani  huku wagonjwa 21 wakikutwa pia na vimelea vya malaria.
“Kinondoni ndiyo iliyokuwa na wagonjwa wengi ambayo ilikuwa ni asilimia 48.5 wenye maambukizi na wagonjwa wengi walikuwa ni wenye umri miaka 15 hadi 44 hasa wanaofanya kazi nje ya maeneo yao ya kuishi huku kundi hili likiwa katika hatari ya maambukizi mara tatu zaidi ya makundi mengine.
Alisema utafiti huo umebainisha kuwa wengi wa wagonjwa wa Dengue walikuwa ni wale ambao wametumia au waliokuwa wanaendelea kutumia dawa za kutibu malaria.
Malecela alisema kutokana na matokeo hayo ni vyema ukaanzishwa mpango wa kufuatilia ongezeko la mbu katika jiji ili kuweza kutabiri uwezekano wa milipuko ya Dengue katika siku zijazo.
“Kwa kuwa wagonjwa wengi waliokuwa na maambukizi mseto ya malaria na Dengue, hivyo kunahitajika kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa yanayoambatana na homa husani wakati wa majira ya mvua,” alisema.

No comments: